Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 12:42 pm

NEWS: TUME YA UFILISI YAPENDEKEZA KUWEPO SHERIA MOJA YA UFILISI

Tume ya Kurekebisha Sheria imependekeza kutungwa kwa sheria moja itakayosimamia masuala ya ufilisi nchini kutokana na kuwepo na changamoto mbalimbali utoaji wa adhabu ndogo.
Pendekezo hilo limekuja baada ya kubaini zipo sheria za ufilisi ambazo zimepitwa na wakati na baadhi zinatoa adhabu au faini ndogo kwa wale wanaokiuka taratibu za ufilisi kama vile Sh.200 au Sh.1,000.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu January Msoffe alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akiwasilisha ripoti ya mapitio ya Sheria zinazosimamia mfumo wa ufilisi Tanzania kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Augustine Mahiga.

Jaji Msoffe alisema utafiti wao umebaini hadi sasa hakuna sheria mahususi inayosimamia masuala ya ufilisi nchini.

Alisema masuala hayo yamekuwa yakisimamiwa na sheria mbalimbali za kisekta kama vile Sheria ya Makampuni sura ya 212, Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Sura ya 342, Sheria ya Vyama vya Ushirika Sura ya 211, Sheria ya Ufilisi, Sheria ya Bima Sura ya 394, Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Usajili wa Wadhamini sura ya 318.

Jaji Msoffe alisema kuwepo kwa sheria hizo kunasababisha mkanganyiko kwa watumiaji kwa kutojua ni sheria ipi inayopaswa kutumika ili kutatua tatizo linalowakabili.

“Kuwepo kwa Sheria hizi kumesababisha ugumu kwa wadai kujua utaratibu wa kutumia kupata haki zao kwa wakati mara baada ya kampuni au taasisi husika kufilisika, pia kumesababisha uwepo wa taratibu ndefu na hivyo kuchelewesha mashauri ya ufilisi kumalizika kwa wakati,”alisema.

Alifafanua kuwa faini ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye sheria hizo haziendani na kiwango cha kiuchumi cha maisha ya sasa.

“Baadhi ya Sheria hizo, zinatoa kiwango kidogo sana cha mtaji ili kampuni au taasisi ionekane kuwa imefilisika, pia sheria hizi zinatambua njia moja ya mawasiliano mfano kwa njia ya posta,”alisema.

Alisema hali hiyo inafanya sheria hizo kutoendana na maendeleo yaliyopo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na hivyo kuna haja ya kuzirekebisha ili ziendane na mazingira ya sasa.

Aidha, alisema utafiti umebaini kwamba Mahakama zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinasababisha ucheleweshaji wa usikilizaji na kumalizika kwa mashauri kwa wakati.

“Mfano, shauri ya Tritel tangu kufunguliwa kwake mahakamani mwaka 1999 hadi leo halijaisha,”alisema.

Kadhalika, alisema wamebaini kwa mujibu wa Sheria za Tanzania kampuni inapofilisika wanaopewa kipaumbele kulipwa haki zao ni walio na madeni na si wafanyakazi.