Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 10:48 am

NEWS: TUME YA UCHAGUZI YARUHUSU KUTUMIA VITAMBULISHO VINGINE KUPIGA KURA

Dar es Salaam: Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeruhusa matumizi ya vitambulisho mbadala kwenye uchaguzi mdogo wa kata tatu, uliopangwa kufanyika kesho Januari 19, 2019. Akizungumza leo Ijumaa Januari 18, Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesema Tume imetoa ruhusa hiyo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62(a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jaji Kaijage amesema jumla ya wapiga kura 26,282 katika vituo vya kupigia kura 69 watahusika na uchaguzi huo mdogo wa udiwani.

“Tume imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura, zimeharibika au zimechakaa watumie mojawapo ya vitambulisho ikiwemo pasi ya kusafiria, leseni ya udereva au kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida),” amesema Jaji Kaijage. Amesisitiza kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika.

Jaji Kaijage amesema kwamba tume imewaelekeza watendaji wa uchaguzi vituoni wawape kipaumbele wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee.

Pia ameelekeza kwamba mpigakura mwenye ulemavu wa kutoona, ataruhusiwa kwenda kituoni na mtu atakayemchagua mwenyewe kwa ajili ya kumsaidia kupiga kura. “Wapiga kura wanatakiwa kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na wajiepushe na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia kura,” ameagiza. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika katika kata ya Magomeni kwenye halmashauri ya manispaa ya Kinondoni, kata ya Mwanyahina iliyopo halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu na kata ya Biturana katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma