Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:45 am

NEWS: TIZEBA: WALIOSHISHWA MALENGO MIRADI YA KILIMO WAKAE BENCHI

MOROGORO: WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewataka viongozi wa miradi ya kilimo inayofadhiliwa na serikali na mashirika ya misaada, kuzingatia malengo ya kuanzishwa miradi hiyo ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, na kwamba kama kuna asiyeweza, ni bora apishe wengine.

Akizungumza katika siku ya umwagiliaji ya Dakawa mkoani Morogoro hivi karibuni, Dk Tizeba alisema wakulima hawana sababu ya kuwa na hiyari, kwani fedha zinazotolewa ni nyingi na wahisani pamoja na serikali wanataka kuona matokeo ya misaada hiyo. “Waliopewa pesa kwa ajili ya kilimo wasiwe na hiyari ya kulima, hatuwezi kuendelea kusikia tu wenzetu wanavuna tani nyingi katika mataifa mengine ikiwa sisi bado tunaendelea hivihivi,” alisema na kusisitiza: “Anayetaka kukaa hapa kwenye skimu akae kwa kufuata masharti na asiyetaka aondoke apishe wengine.

USAID (Shirika la misaada la watu wa Marekani) kiasi walichotoa kinafikia Sh bilioni 29, tukizigawa kila mmoja anapata Sh milioni 60. Msimu ujao tunataka tuvune tani 12 katika skimu hii.” Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo, Dk Filimini Mizambwa alisema ili taasisi zinazosaidia wakulima ziendelee kuwepo lazima wakulima hasa wadogo waoneshe tija katika shughuli wanazofanya ikiwemo kuonesha matokeo mazuri wakati wa mavuno.

“Ili sisi tuendelee kuwepo lazima wakulima hasa mkulima mdogo afanikiwe, wito wangu wakulima wajifunze kilimo chenye tija na kufanya kazi kwa juhudi ili kuwaonesha wafadhili fedha zao hazipotei bure kwa uzembe,” alisema. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga alisema malengo ya ziara hiyo katika skimu ya umwagiliaji ya wakulima wadogo Mkondo na skimu kubwa ya Dakawa yenye ukubwa wa hekta 2,000 inalenga kuangalia shughuli zinazofanyika na kuangalia changamoto zilizopo. Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa skimu hizo za umwagiliaji mkoani Morogoro utakaofanywa hivi karibuni na Rais John Magufuli.