Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:31 pm

NEWS: TANZANIA YATOA NEEMA KWA MSUMBIJI,ZIMBABWE NA MALAWI.

DAR ES SALAAM: Nchi ya Tanzania kupitia Rais wake Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imedhihirisha ule msemo wa "undugu ni kufaana na si kufanana" baada kujitolea msaada wa vyakula na madawa ili kuwasaidia wananchi walioathirika na mafuriko ikiwa ni sehemu ya kudumisha umoja na ushirikiano baina ya nchi hizi.


Hayo yamejiri leo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi kwa kushirikiana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kutoa msaada wa vyakula na madawa kwa nchi za Msumbiji na Malawi baada yakupata janga la mafuriko.


"Hawa ni ndugu zetu, jirani zetu, tupo pamoja katika jumuia ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC), kwahiyo Tanzania imeona ni vyema katika undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea nchi hizi msaada wa madawa na chakula ikiwa ni sehemu ya kuwapa pole kwa maafa haya" alisema Prof. Kabudi.


Prof. Kabudi amesema kuwa Kimbunga hicho cha Idai kimepelekea mafuriko ambayo yameleta maafa makubwa sana, huku nchi ya Msumbiji jumla ya watu 221 wamepoteza maisha, huku watu 88 kutoka Beira, watu 68 Manika, watu 51 Zambezi, na watu 19 kutoka Tete, huku zaidi ya watu 1000 hawana mahali pa kuishi.


Prof. Kabudi aliendelea kusema kuwa, kwa upande wa Zimbabwe watu 98 kutoka mji wa Manipaland wamefariki, huku watu 122 wakiwa wamefariki katika nchi ya Malawi, huku wengine wakiachwa katika hali ngumu.

Aidha, Prof. Kabudi amewaasa Wafanya biashara na wananchi wengine walioguswa na maafa haya wasisite kutoa msaada kwa nchi jirani ambazo zimepata majanga Hayo kadiri ya uwezo wao.

Pia, Prof. Kabudi aliendelea kuyaasa mashirika, makampuni na watu binafsi ambao wameguswa na hali ambayo imezikuta nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe waweze kuchanga na kuvikabidhisha vitu hivyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya ili viweze kupelekwa mahala husika.


Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara ya Afya imeandaa tani 24, ambazo ni sawa na tani (8) kwa kila nchi ambazo zitasaidia wananchi waliopata janga hilo kukabiliana dhidi magonjwa.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mawaziri wa Afya kutoka nchi za Zimbabwe na Malawi dawa kubwa zinazohitajika ni dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria (antibiotics) na dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, (ORS) na dripu.


"tumeweka takribani aina tano za dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria, tumeweka dawa kwa ajili ya magonjwa ya matumbo, Kama vile kuhara (ORS), tumeweka dawa kwa ajili ya kutibu kwa kutumia maji (dripu), pia mashuka, magodoro, vyandarua, blanket na dawa za maumivu " alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa kila nchi itapata tani saba (7) za mchele kwa ajili ya Msumbiji na Zimbabwe na Malawi watapata tani 200 za mahindi ambayo yatatoka katika mkoa wa Mbeya ambayo upo karibu na nchi hiyo.

Kwa upande wa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Glad Chembe Munthali ameishukuru nchi ya Tanzania kwa upendo na msaada waliouonesha kwa Malawi na kuahidi kufikisha salam hizo za upendo kwa rais wa Malawi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania na ya Malawi zitaendelea kuwa marafiki milele.