Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:25 am

NEWS: TANZANIA YATABIRIWA MAKUBWA KIUCHUMI

TANZANIA inakaribia kufanya kilichofanywa na Ethiopia mwaka 2015 kwa kuipiku Kenya katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa kiwango cha ukuaji uchumi miongoni mwa nchi za eneo la Afrika ya Mashariki.

Kwa miaka mitano iliyopita, uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa asilimia saba, lakini waKenya umekuwa ukiongezeka kwa asilimia tano. Benki ya Dunia (WB) inakadiria kuwa, mwakani uchumi wa Tanzania utashika nafasi ya tatu kwa kiwango cha ukuaji barani Afrika, nyuma ya Ethiopia na Ghana. Kwa mujibu wa WB, mwakani uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2, Ghana asilimia 7.8 na Ethiopia utakuwa kwa asilimia 8.3. Kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi la Kimataifa (WEF) Tanzania inashika nafasi ya tano miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonesha kuwa, kwenye miaka 20 iliyopita, uchumi wa Tanzania umeongezeka mara saba, lakini tangu mwaka 1997 uchumi wa Kenya umekua mara tano na huenda kwenye miaka ijayo hali itaendelea kuwa hivyo. Kwa mujibu wa takwimu hizo, kuna wakati uchumi wa Kenya ulikuwa mkubwa mara nne kuliko wa Uganda lakini pengo hilo sasa linapungua.

Miaka 20 iliyopita uchumi wa Kenya ulikuwa mkubwa mara 20 zaidi ya ule wa Tanzania lakini pengo limepungua kwa zaidi ya nusu. Takwimu za IMF zinaonesha kuwa, mwaka 1997 pato ghafi la taifa (GDP) la Kenya lilikuwa Dola bilioni 13.7 za Marekani, na GDP ya Tanzania ilikuwa Dola bilioni 6.4 za Marekani. Kwa kuzingatia takwimu hizo, uchumi wa Kenya ulikuwa mkubwa mara 114 kuliko wa Tanzania.

Mwaka jana, uchumi wa Kenya ulikuwa mkubwa mara 46 kuliko wa Tanzania hivyo pengo linazidi kupungua. Takwimu za IMF zinaonesha kuwa, kwenye miaka 20 iliyopita GDP ya Kenya imekuwa mara tano na kufikia Dola bilioni 68.9 za Marekani na unatarajiwa kufikia Dola bilioni 75 mwaka huu. Kwenye muda huo, uchumi wa Tanzania umekua mara saba na kufikia GDP ya Dola bilioni 47.1 mwaka jana.

Tangu mwaka 1987 Kenya imekuwa ikiongoza kwa kiwango cha ukuaji uchumi na kuzishinda Tanzania, Uganda na Rwanda. Takwimu za IMF zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 1982 hadi 1984 Tanzania ilikuwa na uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo la mashariki ya Afrika. Mwaka uliofuata Kenya ilichukua nafasi hiyo, lakini mwaka 1986 Tanzania ilirudi kwenye nafasi yake, lakini mwaka 1987 Kenya ikawa juu tena hadi sasa.

Kwa mujibu wa wataalamu, kasi ya uchumi Tanzania inaongezeka kwa kuwa nchi inatumia sera za uchumi wa soko badala ya zile za ujamaa. Mwaka jana mchumi wa Kenya, David Ndii alisema, kama Tanzania itaendelea na kasi ya sasa, ifikapo mwaka 2021 itakuwa namba moja kwa ukubwa wa kiwango cha GDP. “Tanzania inakaribia kuipiku Kenya kwa kiwango cha uchumi.

Kwenye miaka mitano, na kiwango cha sasa cha ukuaji kitaendelea, uchumi wa Tanzania utakuwa kwa asilimia 20 kuliko wa kwetu (Kenya)” alisema mapema mwaka jana. Hata hivyo, takwimu za makisio ya IMF yanaonesha kwamba, ifikapo mwaka 2022, uchumi wa Kenya utafikia Dola za Marekani 113, wa Tanzania utakuwa Dola za Marekani bilioni 78 hivyo kumaanisha kwamba, itachukua muda zaidi kwa Tanzania kuipiku Kenya. Sekta binafsi Kenya inafanya vizuri zaidi na ni injini ya uchumi wa nchi hiyo zikiwemo kampuni za Kenya zilizowekeza Tanzania.

Inakadiriwa kuwa muda mrefu uliotumika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu Kenya, ukame na mipango ya kuuza mafuta nje yamepunguza kiwango cha matarajio na huenda kasi ya ukuaji ukawa ndogo zaidi kulinganisha na kiwango cha miaka mitano iliyopita.

Tanzania imekuwa mzalishaji mkubwa wa dhahabu na almasi, ina gesi ya asili na helium, inajenga reli yenye kiwango cha kimataifa, inashirikiana na Uganda kujenga bomba la mafuta ghafi kuyapeleka bandari ya Tanga na inapanua bandari zake kuiwezesha kuingiza bidhaa ambazo awali ilizinunua Kenya. Tanzania imeboresha usafiri wa abiria katika mji wake wa kibiashara wa Dar es Salaam kwa kutumia mabasi 140 yaendayo kasi (BRT) ambayo hadi sasa yanatumia barabara zenye urefu wa kilomita 21, vituo vikuu vitano, na vituo 27 vya kusubiria magari hayo.