Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 5:54 pm

NEWS: TANZANIA YASISITIZA KUWA HAKUNA EBOLA NCHINI HUMO

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amethibitisha kuwa nchi yake haikuwapatia Shirika la Afya Duniani (WHO) sampuli za vipimo vya wagonjwa wawili walioshukiwa kuwa na virusi vya Ebola, kwa kuwa vipimo vya ndani vilithibitisha kuwa watu hao hawakuwa na ugonjwa huo.

Mwishoni mwa Mwezi Septemba, WHO ilitoa taarifa ambayo iliilaumu Tanzania kwa kutokutoa ushirikiano juu ya uchunguzi wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na dalili zinazofanana na za Ebola.

Chini ya kanuni za Afya za kimataifa, makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama, nchi zinalazimika kuiarifu WHO mara tu zitakapokuwa na milipuko ya magonjwa makubwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kuwa hatari kwa majirani zao na ulimwengu.

"Kwanza kusema kweli nashangaa kwa nini WHO walitoa taarifa ile," ameeleza Ummy na kuongeza: "Ili sampuli iende WHO, inabidi kwanza vipimo vya ndani viwe positive (chanya), na sisi tulikuta ni negative (hasi) pili inatakiwa ufikishe watu 25, na sisi kulikuwa na kesi za washukiwa wawili tu."

Waziri Mwalimu amesisitiza kuwa Tanzania haina uwezo wa kuficha ugonjwa wa Ebola.

"Ni Mgonjwa hatari, unaambukiza na kuua kwa haraka sana… Tunasisitiza kuwa haupo nchini na endapo ukithibitika kuingia tutatimiza wajibu wetu kwa kuitaarifu WHO."

Bi Mwalimu anasema taarifa zinazoenezwa dhidi ya Tanzania zinaifanya serikali kuamini kuwa kuna njama za makusudi za kuichafua nchi hiyo zinazofanywa kwa makusudi.

Presentational white spaceTayari nchi za Marekani na Uingereza zimeshatoa angalizo kwa raia wake wanaopanga kuzuru Tanzania kuchukua tahadhari juu ya tishio la maambukizi.

Mlipuko wa Ebola unaendelea kushika kasi Mashariki mwa nchi jirani ya Tanzania ya DRC na tayari zaidi ya watu 2,000 wamepoteza Maisha toka mwaka 2018.

Waziri Mwalimu amekiri kuwa uwepo wa ugonjwa huo Mashariki mwa Congo kunaleta tishio kubwa kwa Tanzania kutokana na muingiliano wa raia wan chi hizo mbili.

"Tunachukua hatua madhubuti maeneo ya mipakani kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoingia Tanzania wanapimwa…Tumejiandaa kwa vifaa kinga na tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu juu ya kutambua dalili na namna ya kujikinga na kutoa taarifa kwa haraka pale watakapoona mtu mwenye dalili," amesisitiza.