Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:27 am

NEWS : TANZANIA YAKOPESHWA MABILIONI YA FEDHA SEKTA YA UTALII

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeipatia Tanzania mkopo wa Dola za Marekani 150 milioni sawa na Sh336 bilioni kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii wa asili katika maeneo ya mikoa ya kusini mwa nchi.

Fedha hiyo ilitolewa na Shirika la maendeleo la kimataifa la benki hiyo (IDA) kupitia mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa ajili ya utalii (REGROW) baada ya kuidhinishwa wiki iliyopita.

Fungu hilo litakalotumika kwa miaka sita, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, litazinufaisha kiuchumi kaya takriban 40,000 zilizopo katika hifadhi kwa kuwa kutajengwa miundombinu na fursa mpya za kiuchumi kwa lengo la kuongeza usimamizi wa hifadhi za asili.

Mpango huo una lenga kukuza uhifadhi wa mapori ya Taifa, mbuga, maporomoko ya mto Ruaha na kupunguza mwingiliano wa kimakazi kati ya binadamu na wanyama pori.

Maeneo yatakayohusika na mpango huo ni Mbuga za Katavi, Kitulo, Mahale, milima ya Udzungwa, Mikumi na Ruaha, Pori la Selous, Mito inayopitiwa na bonde la ufa (Nyansa na Tanganyika) .

Kuhusu Mpango huo, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa nchi za Tanzania, Malawi, Somalia na Burundi, Bella Bird alisema utalii ni eneo muhimu kwa maendeleo ambalo linaweza kuongeza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa asilimia 10 ya pato la Taifa (GDP) kwa hesabu za mwaka 2015.

“Nchi hii imejaliwa wanyama wengi na vivutio vya asili lakini vinavyotambuliwa na kujulikana zaidi ni vile vya maeneo ya Kaskazini mwa nchi. Kuanza kuyajali maeneo haya ya kusini kutaongeza idadi ya watalii, hivyo kuongeza faida za kiuchumi,” alisema Bird.

Alisema Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi kubwa ya watalii ndani ya muda mfupi kutoka watalii 500,000 kwa mwaka 2000 hadi watalii zaidi ya milioni moja kutokana na kuvitangaza vivutio vyake.

“Ukaichilia mbali sifa ya kutunza vivutio, Serikali inapata mapato na sekta hii hutoa ajira nyingi, mpaka sasa Tanzania ni zaidi ya watu 400,000 walioajiriwa katika sekta hiyo,” alisema Bird.

Kwa upande wake mtaalamu wa mazingira wa Regrow, Daniel Mira alisema endapo eneo hilo la kusini litafanywa kuwa maalumu kwa vivutio Tanzania itakuwa imejiimarisha katika utalii.

“Hata mapato yatakayokuwa yakipatikana yatakuwa na uwezo wa kuendeleza vivutio vya kipekee jambo ambalo litalifanya eneo hilo kuwa kitovu cha ukuaji wa kikanda na la mfano,” alisema Mira.