Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:45 am

NEWS: TANZANIA YAKASIRISHWA TAARIFA YA NTV YA VIFO VYA WATU 50

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ndio Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amekijia juu chombo cha habari cha NTV kwa kutoa taarifa alizodai kuwa za uzushi kuhusiana na maendeleo ya ugonjwa wa Corona nchini.

Mitandao yao ya Kijamii ya Twitter na facebook ya NTV waliweka taarifa inayosema idadi ya watu waokufa siku ya jana Alhamisi Aprili 30,2020 kwa ugonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam ni 50 jambo ambalo Dk Abbas amelikanusha akisema ni uongo.

ujumbe wa taarifa hiyo ya NTV ilisomeka kuwa " Watu 50 wamekufa leo jijini Dar es Salaam kwa maambukizi ya Corona, Kiongozi Mkuu wa Upinzani Tanzania siku ya Jumatano aliishutuma serikali kwa kuficha taarifa sahihi za ugonjwa huo na kushindwa kuchukua tahadhari ya kudhibiti maambukizi," Hii ndio taarifa iliyowekwa na NTV kwenye mtandao wao wa Twitter na facebook

Sasa baada ya taarifa hiyo kusambaa, Dk Abbas ameishutumu NTV kwa kuripoti taarifa hiyo ambayo siyo sahihi huku akiwakumbusha kufuata misingi ya taaluma ya habari.

" Huu ni Uandishi au Uhandisi wa habari? Inasikitisha kuona jinsi NTV Kenya inavyokua wakala wa uongo na uzushi. Nawakumbusha wazandiki hawa kuenzi misingi ya taaluma badala ya umaamuma," Imesomeka hivyo taarifa ya Dk Abbas aliyoiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Ikumbukwe jukumu la kutoa taarifa ya maendeleo ya ugonjwa wa Corona inatolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa au Rais Dk John Magufuli.