Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 2:14 am

NEWS: TANGAZO LA KUHUISHA MIKATABA YA IPTL YAMTOKEA PUANI MKURUNGEZI MKUU EWURA

DAR ES SALAAM: UTATA wa maombi ya kuzalisha umeme ya kampuni ya IPTL yamesababisha kibarua cha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi kuota mbawa baada ya kusimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Habari za kusimamishwa kazi kwa Ngamlagosi zilitolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu usiku wa kuamkia jana. kwenye taarifa hiyo hazikutolewa sababu za kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo, lakini hata hivyo imebainika kuwa utata wa kile kilichoitwa maombi ya IPTL ya kuomba kuzalisha umeme ndio chanzo cha kusimamishwa kwake kazi. “Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Felix Ngamlagosi. Amesimamishwa kazi kuanzia leo (jana),” ilisema taarifa hiyo fupi iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.

Wakati Ikulu inatoa taarifa hiyo, Ewura kwa upande wake ilikuwa imetoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuonesha kusitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya mwombaji, ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni, mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine. “Taarifa inatolewa kwa umma kwamba kufuatia mambo ya kampuni ya uzalishaji umeme ya IPTL kuomba kuongezewa leseni yake ya kuzalisha umeme kwa kipindi cha miezi 55, kutokea tarehe 15 julai 2017 Ewura, zaidi ya hatua nyingine za kiudhibiti, iliwasiliana na wizara ya nishati na madini ili kupata maoni yake kwa mujibu wa kifungu cha 7(3) cha shreia ya Ewura.

“Wizara ya nishati na madini imetoa mapendekezo ya kuwapo na mashauriano zaidi kati ya wizara, ewura na wadau mbalimbali wa sekta ndogo ya umeme, kabla ya kuendelea na mchakato wa maombi ya mwombaji. Kutokana na maoni hayo, Ewura inasitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya mwombaji ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni, mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewea maelekezo mengine,” ilisema taarifa hiyo ya Ewura.

Haijajulikana sababu za Ewura kusitisha mchakato huo haraka namna hiyo wakati ilikuwa kwenye mikakati ya kuhamasisha wadau kuwasilisha maoni yao kuhusu maombi hayo ya IPTL. Kampuni ya IPTL inamilikiwa kwa ubia na Pan Africa Power Solutions (T) ltd, Euroasia Holding Ltd na Hi Tide Trade Ltd. Kuanzia wiki iliyopita, Ewura ilitoa matangazo kwenye vyombo vya habari ambayo ilikuwa ni taarifa kwa umma kwamba mamlaka hiyo imepokea maombi ya kuongeza muda wa leseni ya kuzalisha umeme kutoka kwa kampuni ya uzalishaji umeme ya IPTL.

“Hivyo basi Ewura inauarifu umma na wadau mbalimbali kwa ujumla kuwasilisha maoni au pingamizi ili kufanikisha uchambuzi mzuri wa maombi haya,” lilisema tangazo hilo la Ewura. Mamlaka hio iliwataka wananchi kuwasilisha maoni hayo kwa maandishi na mwisho wa kupokea maoni hayo ilikuwa ni Juni 30 mwaka huu. Pamoja na tangazo hilo, Ijumaa Ewura iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kufafanua juu ya maombi hayo ya IPTL baada ya watu wengi kuonesha kulalamikia kupitia mitandao ya kijamii baada ya kuwepo taarifa kuwa tayari IPTL wameishaipatia leseni kampuni hiyo.

“IPTL haijapewa leseni kama watu wanavyoaminishwa, bali mamlaka hiyo ilitoa taarifa kwa umma ikiomba maoni kuhusu ombi la IPTL kuongeza leseni ya uzalishaji wa umeme,” alisema Meneja Mawasiliano wa Ewura Titus Kaguo. Kaguo alifafanua kuwa “Watu wamekuwa wakilalamikia mikataba, hali fulani ya umeme na mikataba ilivyoingizwa, ndio maana tunatarajia watu walete maoni na mapingamizi, ifikie wakati tujadili mambo kwa mustakabali wa taifa na taifa ya vizazi vijavyo, hii ya kuanza kulalamika inaweza isitusaidie.”

Juzi jioni Mkurugenzi wa Sheria wa Ewura, Edwin Kidiffa alifanunua kupitia kituo cha runinga cha taifa (TBC1) ambako alisema Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa kilichoko mbele ya mamlaka hiyo ni maombi ya kuongeza muda wa leseni ya IPTL na sio vinginevyo. Ngamlagosi aliteuliwa na Bodi ya Ewura kuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Februari mwaka 2014. Alishika wadhifa huo kutoka kwa Haruna Masebu ambaye alimaliza mkataba wake Desemba 2013.

Ngamlagosi ambaye ana shahada ya uzamili kwenye masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Fedha cha Moscow, kabla ya kuwa mkurugenzi mkuu alikuwa mkurugenzi wa uchumi wa mamlaka hiyo. Mkataba wa IPTL na Tanesco IPTL ni miongoni mwa wazalishaji ambao wamekuwa wanalalamikiwa na Watanzania kuingia mkataba mbovu na Shirika la Umeme (IPTL). IPTL inachakata umeme kwa kutumia mafuta mazito na imekuwa inaiuzia umeme Tanesco kwa bei ya juu. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwahi kusema “Nakiri kuwa deni la Tanesco ni kubwa.

Na hii inatokana na mikataba mibovu, rushwa na uongozi dhaifu. Na ndugu zangu Watanzania niwaeleze, mtu asije akawaeleza unafuu wa kampuni yoyote inayoiuzia umeme Tanesco sasa hivi, haipo, labda tu (mtu) awe ametumwa kuishabikia.” Profesa Muhongo alisema “Tutasema ukweli mbele ya Mwenyezi Mungu, mikataba yote si mizuri… sasa nimechukua hapa mifano, Songas tulikuwa tunalipa ‘capacity charge’ kwa mwezi dola za Marekani milioni 4.6, Symbion dola milioni 2.4, IPTL dola milioni 2.6, Aggreko dola milioni mbili. Nawaomba waheshimiwa wabunge, msitumike kuja hapa kuishabikia.” Kutokana na ubovu wa mikataba na IPTL kuikamua Tanesco, baadhi ya wabunge waliwahi kupendekeza kuwa Serikali itaifishe mitambo ya IPTL mara mkataba wake utakapomalizika.