Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 4:55 am

NEWS: TAMISEMI YAOKOA MILIONI 100 BAADA YA KUFANYA VIKAO KWAJIA YA VIDEO

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima ametumia mfumo wa uendeshaji wa vikao vya kazi kwa njia ya kielektroniki yaani “video conferencing” na kufanikiwa kuokoa zaidi ya milioni 100 wakati akifanya mkutano na Wajumbe 234 wa Timu za Uendeshaji Huduma za Afya Mikoa, Wakurugenzi na Walezi wa Mikoa kutoka OR-TAMISEMI.

Mkutano huu ambao umefanyika kwa teknolojia hiyo ni wa mara ya kwanza na unalenga kupunguza gharama za safari kwa ajili ya vikao ambavyo, ajenda zake zinaweza kujadiliwa kwa njia ya kielektroniki na hivyo kuboresha ufanisi katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Akiongea kwa njia ya Video Conference kutokea Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa kwenye ziara ya kikazi, Dkt. Dorothy Gwajima amesema, kuanzia sasa atakuwa akitumia njia ya kielektroniki “Video Conference” kwa ajili ya kuwakutanisha wadau wote wa sekta ya afya kujadili masuala yanayowahusu pia kutoa maelekezo na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu.

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa iwapo angefanya kikao cha siku moja cha wadau hao wa afya , posho peke yake bila gharama za safari na ukumbi kwa siku moja ingegharimu takribani Tsh. milioni 30 na ukijumlisha na siku 2 za safari kuja Dodoma ingeweza fikia siyo chini ya Tsh. Milioni 100 au zaidi.

Anaendelea kufafanua kuwa, mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya kieletroniki (video conference) utasaidia kudhibiti matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo na kuwezesha kusaidia kutoa maagizo ambayo yatasaidia kufanya maboresho ya haraka na kuleta tija katika Sekta ya Afya nchini.

Amesema kuwa, kufanya vikao kwa kutumia mfumo huo kutasaidia kutatua changamoto zilizopo katika Mikoa na Halmashauri kwa kutoa ushauri wa haraka na kupokea taarifa za utekelezaji kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na gharama za safari kwa ajili ya kufanya vikao.

Related image

Wakati huohuo Dkt. Dorothy Gwajima amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Timu za Uendeshaji Huduma za Afya nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina ili, kubaini changamoto wanazozisema kwa takwimu siyo kwa maneno tu ya jumla ambayo yanayoficha uhalisia wa changamoto husika.

“Kabla hatujasema upungufu wa watumishi tufanye mahesabu ya uwiano wa uwingi wa kazi kwa kila mtumishi kwa kutumia fomula ya WISN ambayo, tumefundishwa wote. Vinginevyo ukisubiri hadi Wizara ije ifanye basi hapo ni kwamba, RHMT/CHMT mtakuwa mmeshindwa kutekeleza wajibu wenu na badala yake mmegeuka chanzo cha changamoto” Amefafanua Dkt. Gwajima.

Dkt Gwajima amaesisitiza kufanya hesabu sahihi ili kuweza kuwapata baadhi ya wataalamu na kuwahamisha waende kwenye upungufu mkubwa zaidi wakati, zoezi la ajira likiendelea.

Vilevile, Dkt. Gwajima amewataka wajumbe hao kuhakikisha kabla ya kuandika changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba, ni vyema wakahakiki maeneo yenye akiba ya vifaa ambavyo havitumiki ili vipelekwe maeneo yenye uhitaji mkubwa badala ya kila mara tunawaza kununua hivyo kusababisha baadhi ya vifaa kuharibika au kupotea.

Aidha amezitaka RHMT kumiliki taarifa wanazotuma Wizarani na kuhakikisha wanazituma kwa wakati kwa kuwa , kila mmoja atatetea taarifa aliyoituma kupitia vikao hivyo na uwajibikaji wake utawekwa wazi ambapo kwa sasa vikao hivyo vitakuwa vitafanyika kila mwezi kwa pamoja na kila wiki kutakuwa na ratiba ya mikoa kadhaa kuhudhuria vikao hivyo na kuwasilisha taarifa za maendeleo ya uwajibikaji.

Wakati huohuo Waganga Wakuu wa Mikoa wameupongeza mpango wa kuendesha vikao kwa njia ya Kielektroniki ambao umesaidia kutoa mtazamo mpya wa jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za Sekta ya Afya nchini.