Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:34 am

NEWS: TALGWU KUISHTAKI SERIKALI

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kinatarajia kufungua kesi kuishtaki Serikali kwa madai ya kuwaondoa watumishi 2,115 kinyume na utaratibu.


Kabla ya uamuzi huo, chama hicho kimeiomba Serikali kuwarejesha kazini watumishi walioajiriwa kupitia cheti cha elimu ya msingi ya darasa la saba.


Katibu Mkuu TALGWU, Rashid Mtima alisema watumishi hao walifukuzwa kazi na kusimamishwa mishahara yao kinyume na tangazo.


Mtima alikuwa akifungua mafunzo ya semina elekezi kwa viongozi wa matawi yote ya Halmashauri Mkoa wa Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.


Alisema chama hicho kinasikitishwa na mwenendo wa Serikali kukaa kimya tangu vilipofanyika vikao vya pamoja vya kuwarudisha watumishi kazini.


Alisema idadi hiyo ni kubwa na imeathiri watumishi wa Serikali za Mitaa kwenye sekta ya afya kwa asilimia 69, watumishi wa afya 27, maji na asilimia iliyobaki ni kwa watumishi wengine wakiwamo maofisa watendaji wa vijiji.


“Vikao vinne tumefanya nao sasa inatosha, tayari tunakwenda mahakamani ingawa hatutetei watu wanaoghushi.


“Si kwa kundi hili ambalo Serikali imeliondoa hawakupewa chochote na wala hawaambiwi jambo lolote huku wakibaki kuhangaika jambo ambalo uongozi wa chama umeapa kutokaa kimya,”alisema Mtima.


Alisema watumishi wanaowapigania kurudi kazini ni wale walioajiriwa kabla ya Mei 20, mwaka 2004 ili warejeshwe kazini kwa sababu tayari wamewasilisha vyeti vyao vya kujiendeleza na elimu ya kidato cha nne.


Serikali ilisimamisha ukaguzi wa watumishi wa umma wenye kiwango cha elimu ya darasa la saba Julai, 11 mwaka huu na watumishi hao walitakiwa kuwasilisha serikalini vyeti vyao vya kujiendeleza.


Alisema watumishi hao waliweza kuwasilisha vyeti vyao sehemu husika lakini hadi sasa Serikali hawajaweza kuwarudisha katika vituo vyao vya kazi.


Aliwaomba watumishi wa chama hicho waliopata tatizo hilo kuwa na subira wakati suala lao linafanyiwa kazi.


Kuhusu semina hiyo, Mtima alisema itawajengea uwezo na misingi mizuri itakayowasaidia katika utendaji wao wa kila siku.


Alisema ili kutimiza lengo la kufanya kazi vizuri, ni vema watumishi hao wakafuatilia kwa makini mafunzo hayo waweze kuongeza uelewa.