Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 6:15 pm

NEWS: SPIKA WA BUNGE MAREKANI APANGA KUMUONDOA MADARAKANI TRUMP

Spika wa bunge la Marekani m-Democrat Nancy Pelosi ametangaza rasmi kuanzisha uchunguzi wa kutaka kumuondoa mamlakani Rais wa Marekani Donald Trump na shutuma kwamba aliiomba serikali ya nje kusaidia juhudi zake za kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu Marekani 2020.

Pelosi alitoa tangazo hilo baada ya kukutana ndani ya jengo la bunge na viongozi wa Democratic huku wabunge kadhaa wa chama hicho ambao wanaunga mkono kufunguliwa mashtaka ya kumuondoa madarakani Trump wameendelea kuongezeka kwa siku ya Jumanne.

Pelosi alisema “hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa na rais zimekiuka katiba ya nchi. Rais lazima awajibishwe. Hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria.”

Kwa miezi kadhaa Pelosi amesita kufungua rasmi mashtaka ya kumuondoa madarakani Rais Trump kufuatia shutuma za awali za kuingilia kati sheria kuchukua mkondo wake kutoka kwenye ripoti ya mwendesha mashtaka maalumu Robert Mueller juu ya Russia kuingilia kati uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2016.

Lakini katika siku za karibuni shinikizo limeongezeka kwa Pelosi kufuatia ripoti kwamba Trump alimtaka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kumchunguza mgombea urais wa Democratic na Makamu Rais wa zamani Joe Biden juu ya ajira yenye malipo ya juu aliyokuwa nayo mtoto wake wa kiume Hunter Biden katika kampuni moja ya gesi ya Ukraine.

Biden amekuwa mgombea anayeongoza kwa uteuzi wa urais kupitia Democratic na mpinzani anayeweza kumkabili Trump katika uchaguzi wa 2020.

Trump alisema atatoa Jumatano taarifa kamili ya maandishi iliyorekodiwa juu ya mazungumzo yake ya simu mwezi Julai na Rais Zelenskiy.

Lakini Pelosi na wa-Democratic wengine wanasema kuna mengi kwenye shutuma hii dhidi ya Trump zaidi ya mazungumzo ya simu.