Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:36 am

NEWS: SHIRIKA LA SAVE THE CHILDREN LATUA DODOMA.

DODOMA: Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kutekeleza mradi wa awamu ya pili wa miaka minne ili kumaliza tatizo la kuzaliwa kwa watoto wenye udumavu na uzito pungufu.

Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi wa lishe endelevu wa Shirika la Save The Children Dk. Joyceline Kaganda katika zoezi la kuukabidhi mradi wa lishe endelevu mkoa wa Dodoma unaotajwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu na utapiamlo.

Dk Kaganda amesema Mradi huu utakaogharimu dola Milioni 19.7, utakaotekelezwa hadi mwaka 2022, katika mikoa minne ambayo ni Dodoma, Morogoro, Iringa na Rukwa.

Akiendelea kufafanua Dk Kaganda amesemakuwa mradi huo utajikita zaidi kwenye kutoa elimu kwa jamii hasa wanandoa ili kufanya maandalizi bora kabla na baada ya ujauzito ili kuepusha matatizo ya watoto kuzaliwa na udumavu pamoja na uzito pungufu.

Mbali na hayo Dk. Kaganda amekiri kuwepokwa changamoto hasa kwa kinababa kuamini kuwa masuala ya lishe yanahusu wanawake kwa maana ya kuwa ni mapishi tu jambo ambalo sio sahihi.

Akizungumza baada ya kuupokea mradi huo Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge amesema kuwa bado zipo changamoto hasa katika kubadili tabia kwani haiwezekani katika kipindi cha miaka 58 ya uhuru bado taifa linapambania lishe bora kwa watu wake.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016 ,Tanzania inakabiliwa na tatizo la udumavu wa watoto kwa asilimia 34 huku mkoa wa Dodoma ikiwa ni 36.5% ambapo pia wanawake 2 kati ya 10 katika mkoa huu wakitajwa kuwa na utapiamlo hali inayoelezwa kuwa mbaya katika ujenzi wa taifa imara lenye nguvu kazi ya kutosha.