- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: SERIKALI YATAKIWA KUWALIPA FIDIA WALIOPORWA ARDHI NA CDA
DODOMA: CHAMA cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kanda ya kati kimeitaka serikali kuwalipa fidia wakazi wa Manispaa ya Dodoma ambao kwa namna moja au nyingine wameathirika na vitendo vya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa kuwapora ardhi yao.
Kauli hiyo Imetolewa na Mkurugenzi wa Mafunzo na oganaizesheni wa Chadema, Benson Kigaila wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.
Kigaila amesema kuwa Rais hawezi kuivunja CDA na ikawa ndiyo mwisho wake bila kuangalia madhara yaliyosababishwa na mamlaka hiyo kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka 44 iliyofanya kazi.
Amesema fidia hiyo ni lazima ilipwe na serikali kuu ambayo ndiyo iliyoiweka CDA madarakani na siyo kuliachia jukumu hilo Manispaa ya Dodoma kwa kuwa haihusiki na unyang'anyi huo.
"Kuivunja CDA siyo hoja... Hoja inayokuja hapo ni je wananchi wa Dodoma walionyang'anywa ardhi yao na CDA bila kulipwa fidia watafidiwaje au ndiyo wataachwa waendelee na maumivu yao?" Amesema Kigaila.
Ameongeza kuwa, "Haingii akilini Rais kuivunja CDA na kuacha jukumu la kulipa fidia kwa waathirika walioporwa ardhi yao kwa Manispaa ya Dodoma ambayo haihusiki kabisa katika uporaji huo."
Mbali na hilo amewapongeza wakazi wa Manispaa ya Dodoma pamoja na viongozi wao kwa kupaza sauti kwa nguvu dhidi ya uonevu uliokuwa unafanywa na CDA na hatimaye kupelekea Rais kuivunja rasmi.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Dodoma Makulu (chadema) Paskal Matulaa amesema kuwa sasa ni wakati wa wananchi wa Manispaa ya Dodoma kupata haki yao ya kumiliki ardhi ambayo wameikosa kwa muda mrefu.
Amesema watatumia nguvu ileile waliyoitumia kuing'oa CDA kuhakikisha kuwa Manispaa ya Dodoma inapima ardhi na kuimilikisha kwa wananchi kwa wakati.
Naye Diwani wa kata ya Kizota Yaled Jamal (chadema) amesema wataifanyia kazi kauli ya Rais John Magufuli aliyowataka madiwani wa Manispaa ya Dodoma kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha kuwa ardhi ya Manispaa ya Dodoma inapimwa upya na kugaiwa kwa wananchi kama sheria ya ardhi namba 4 na 5 inavyosema na zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria.