Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 6:48 am

NEWS: SERIKALI YASIMAMA KIDEDEA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI SIMANJIRO

MANYARA: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) George Simbachawene amepokea maoni ya wananchi wa vijiji vya Sukuro na Kityangale kwa ajili ya kutoa suluhu ya mgogoro wa kitongoji cha Katikati kinachogombewa na pande hizo mbili tangu mwaka 2009.

Akitoa maelezo ya awali Mhe. Simbachawene amesema uamuzi wa Serikali utazingatia maslai ya wananchi na nchi kwa ujumla na sio maslai binafsi kama ambavyo makundi makundi yalivyo katika mgogogoro huo wa muda mrefu ambao hauna tija kwa wananchi na maendeleo yao.

“Mimi nimeona na ninachukua maoni yenu bila hata ya kupiga kura, na sitaki kusema nani ameshinda, sawa jamani, acha niende, nitafakari, na nitarudisha majibu ndani ya siku kumi na nne na majibu hayo yatakuwa ndiyo ya mwisho”

Amesema serikali haiwezi kubaki kimya na haiamui, lakini uamuzi wa suala hili utazingatia sana maslai mapana ya wananchi, shughuli za wananchi na Taifa kwa ujumla wala hautaunga mkono kikundi fulani cha watu.

Aidha, alisema uamuzi wa kitongoji cha katikati utazingatia zaidi kuwepo kwa amani na usalama wa eneo lenyewe ili waweze kufanya shughuli za maendeleo na wao wenyewe kwa ujumla.

“Jambo hili ni lazima liishe na litaisha mapema sana, nitakuja kulisema hapa na ndio utakuwa uamuzi wa Serikali. kwa hiyo, mimi nimepokea, uamuzi utakuja ndani ya siku kumi na nne wenye maslai ya watu na maslai ya nchi kwa ujumla,”alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joel Bendera amesema ugawaji wa mipaka mipya ya maeneo hayo itazingatia amani na utulivu kwani historia huko nyuma inaonyesha kuwa kulikuwa na ugomvi ambao hauishi na kuwataka wananchi kusubiri uamuzi wa mwisho wa Serikali.

Mgogoro wa kugombewa kitongoji cha katikati ni wa muda mrefu kwani hata mipaka yake haijawekwa wazi kwa kuwa mazingira ya Maafisa Ardhi kwenda kupima yamekuwa magumu na wameshindwa kwa kuwa jamii hiyo kijiji cha Sukuro, Kityangale na kitongoji cha katikati inayoishi hapo haitoi ushirikiano wa kuonyesha mipaka halisi ya kitongoji hicho ili kila mmoja abaki na eneo kubwa ijapokuwa kitongoji kina eneo kubwa la kutosha kuwa kijiji.

Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene ametembelea shule za sekondari wilayani Simanjiro Loiborsiret na kujionea ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa na maabara ambao umefanikiwa kwa kiwango kikubwa na mwisho alitembelea shule ya sekondari Emboreet yenye kidato cha tano na kuahidi kuwaongezea idadi ya wanafunzi ndani ya muda mfupi.

Pia akiwa shuleni Emboreet ameongea na wazazi, walimu na wanafunzi na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya iwepo ya marafiki wa Shirika la ECLAT Foundation ya Tanzania na Upendo society ya Ujerumani, wakiwemo Foundation for Care and education ya Germany waliotoa fedha za kujenga majengo mbalimbali ya shule hiyo kama shumba za wal;imu na maabara.

Waziri Simbachawene amehitimisha ziara wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa kuiagiza mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Serikali kuendelea kupanda miti na kutunza mazingira kwa maslai ya wananchi na Taifa kwa ujumla.