Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:51 am

NEWS: SERIKALI YANUIA KUTOKOMEZA TB – DKT. ZAINAB CHAULA.

DAR ES SALAAM: Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini, ikiwa ni moja kazi ya malengo ya nchi za SADC ifikapo mwaka 2030.


Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakati akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu na wataalam wa afya wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wakijadili jumla ya ajenda 13 kuhusu masuala ya Afya, hususani HIV/AIDS, Malaria, TB na usambazaji wa dawa.

“Ajenda yetu kubwa ya kwanza, ni kujadili namna ya kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), tunataka inapofika Mwaka 2030 nchi zote zilizo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zinatokomeza ugonjwa wa KIfua KIkuu (TB)”, amesema Dkt. Chaula.

Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa, baadhi ya ajenda zingine zitazojadiliwa katika Mkutano huo, ni masuala ya kutokomeza HIV/AIDS na kutokomeza ugonjwa wa Malaria katika nchi wanachama wa SADC.

Aidha, Dkt. Chaula amesema kuwa, Nchi ya Tanzania, kupitia Bohari kuu ya dawa nchini (MSD) imepewa heshima kubwa katika jukumu la kusambaza dawa, vifaa na vifaa tiba katika nchi zilizo katika Jumuiya ya SADC.

“Nchi yetu ya Tanzania imepewa heshima kubwa ya kusambaza dawa, vifaa na vifaa tiba, kupitia Bohari kuu ya Dawa (MSD) katika nchi zilizo kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika kusini (SADC)”, alisema Dkt. Chaula.

Mbali na hayo, Dkt. Chaula amesema kuwa, masuala ya Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Chanjo ni baadhi ya ajenda zitazojadiliwa baina ya nchi wanachama wa Mkutano huo wa SADC, ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha Sekta ya Afya.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa, takribani watu 200 huambukizwa VVU kwa siku, watu 80 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, huku kati ya hao vijana wanaopata maambukizi, watu 60 ni vijana wa kike.

“Katika Siku moja watu 200 wanaambukizwa VVU, 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, lakini changamoto zaidi ni kwa vijana wa kike, kwa sababu katika vijana 80 wanaopata maambukizi vijana wa kike ni 64, hivyo kama Serikali tunahakikisha kwamba tunawawezesha wasichana walio katika mazingira magumu kiuchumi kupata mahitaji yao ya muhimu na waweze kukaa shuleni”, alisema Dkt. Maboko.

Katika Mkutano huo, wenye wajumbe wa Nchi 16, nchi ya Tanzania imekuwa mwenyeji ikipokea uwenyekiti kutoka nchi ya Namibia.