Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:26 am

NEWS: SERIKALI YAKILI NA KUOMBA RADHI KWA KUWAPIGA WALEMAVU

DODOMA: SERIKALI imeomba radhi na kukiri kuwa nguvu iliyotumika katika suala la waendesha bajaji ambao walikuwa ni watu wenye ulemavu waliopigwa na askari polisi katika jiji la Dar-es-salaam ni kubwa kwa kuzingatia hali zao walizonazo.

Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi MWIGULU NCHEMBA alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum STELLA IKUPA aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusiana na suala hilo.

Akijibu swali hilo NCHEMBA alisema pamoja na kuwepo na ukiukwaji wa utaratibu na kwa kuzingatia hali zao ni kweli nguvu kubwa ilitumika na hivyo kuomba radhi kwa hilo.

Mnamo Juni 16 mwaka huu polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu wenye ulemavu ambao ni waendesha bajaji waliokuwa wameandamana na kufunga barabara ya Sokoine jijini humo.

Watu hao walikuwa na lengo la kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwasilisha malalamiko ya bajaji zao kukamatwa kamatwa na askari wa usalama barabarani.