Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:30 am

NEWS: SERIKALI: ' SI RAHISI AKINA MAMA WAFUNGWA KUPATA MIMBA GEREZANI'

DODOMA: SERIKALI imesema kuwa si rahisi kwa akina mama wafungwa waliofungwa kwa muda mrefu kupata mimba wakiwa gerezani.

Mbali na hilo serikali imejinasibu kwa kueleza kuwa magereza ya wanawake yapo katika kiwango kizuri cha usafi na ubora wa magereza hizo kuwa nzuri zaidi ya magereza za wanaume.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum,Raisa Abdalla Mussa(CUF).

Katika swali la nyongeza la mbunge huyo alitaka kujua ni kwanini kama sehemu ya magereza inaaminika kuwa ni sehemu salama, inakuwaje akina mama wanapata mimba wakiwa gerezani.

Katika swali linguine la nyongeza alitaka kujua ni kwanini serikali isione umuhimu wa akina mama wenye watoto gerezani wasifungwe kifungo cha nje ili watoto wasikae gerezani na watoto wao.

Awali katika swali la msingi la mbunge huyo alitaka serikali imejpanga vipi katika kunusuru watoto ambao hawana hatia.

Mbunge huyo pia amehoji kama serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka magerezani watoto wadogo ambao wanaishi na mama zao waliofungwa wakati watoto hao hawana hatia.

Aidha ametaka kujua kama serikali inaweza kutoa takwimu kwa bunge idadi ya wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita.

Akijibu maswali ya nyongeza Mwigulu alisema hakuna mwanamke yoyote aliyekinzana na sheria na kufungwa kwa muda mrefu ambaye amepatikana na mimba.

Aidha alisema wale wote waliopata mimba ni wale ambao uenda walikinzana na sheria wakiwa na mimba changa.

Hata hivyo amesema kuwa magereza ya wanawake yanaudumiwa na wanawake na kati ya magereza ambayo yapo katika mazingira mazuri ni pamoja na magereza ya wanawake.

Akijibu maswali ya msingi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni alisema kwa muda wa miaka mitano jumla ya wanawake 2,008 walikinzana na sheria na kufungwa gerezani.

Amesema kuhusu watoto kuwepo magerezani na wazazi wao ni kutokana na sheria ya mtoto ya kutaka mtoto kupata haki yake ya kunyonya maziwa ya mama.