Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:38 pm

NEWS: SERIKALI KUPELEKA MAWASILIANO YA SIMU SINGIDA MASHARIKI.

SINGIDA: Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amelielekeza shirika la mawasiliano Tanzania(TTCL)kujenga mnara wa simu katika kijiji cha Msule kilichopo Kata ya Misugha jimbo la Singida Mashariki na kuhakikisha hadi Agosti mwaka huu wawe wamewasha mawasiliano rasmi.


Agizo hilo linafuatia ombi la mbunge wa jimbo hilo Miraji Mtaturu aliyeiomba serikali kupeleka mawasiliano ya simu kwa wananchi.


Akizungumza katika ziara yake ya kikazi jimboni humo ,mhandisi Nditiye amesema serikali imesikia kilio cha wananchi kupitia ombi la mbunge hivyo ni ahadi yao kwao kuwa watajibu ombi hilo kwa wakati.


“Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)imeelekeza serikali kuhakikisha inafikisha mawasiliano kwa wananchi,na serikali yetu chini ya Rais Dokta John Magufuli ni sikivu,hivyo niahidi kwenu kuwa changamoto hii itapatiwa ufumbuzi,”alisema Mhandisi Nditiye.

Awali akitoa ombi hilo Mtaturu amesema wananchi wa Kata za Misughaa,Kikio na Ntuntu wana changamoto kubwa ya mawasiliano ya simu hivyo ni matarajio yao kuwa ombi hilo litasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.



“Mheshimiwa naibu waziri juzi nilikuomba uje ujionee hali ya wananchi wangu ilivyo katika sekta ya mawasiliano,na nashukuru umekubali wito wangu umefika na umeshuhudia simu ulizokuwa nazo mwenyewe hazisomi mtandao wowote,kwa niaba ya wananchi hawa naomba tujengewe mnara ili kurahisisha mawasiliano ya kibiashara na kijamii kwani mawasiliano ndio kichocheo kikubwa cha maendeleo,”alisema Mtaturu.

Aidha upande wa barabara ameiomba serikali kutenga fedha ili kujenga barabara ya njia panda ya Singida kwa Mtoro kupitia Kiblashi hadi Tanga yenye urefu wa kilomita 461 kwa kiwango cha lami.


“Tangu mwaka 2017 serikali imemaliza kufanya upembuzi yakinifu kwenye barabara hiyo,tunachoomba sasa ni kutengwa kwa fedha ili barabara hiyo ijengwe kwa kuwa ni muhimu katika ukuaji wa uchumi kutokana na kugusa mikoa mitatu ya Dodoma,Singida na Tanga,”aliongeza Mtaturu.


Mbali na maombi hayo amemshukuru Rais Magufuli kwa kupeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali kwenye sekta ya elimu,afya na miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mengine ya jimbo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo ameeleza umuhimu wa mawasiliano kiusalama na katika kuchochea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Kwanza nikushukuru Mbunge kwa kumualika kiongozi wetu aje ajionee kwa macho changamoto iliyopo kwenye wilaya yetu,ila tu nikuombe mbali na maeneo uliyoyataja,utusaidie pia kwenye maeneo mengine kama ya Ighombwe,Mgungira na Iyumbu ambako nako pia mawasiliano ni shida,”alitoa ombi Mpogolo.

Katika ziara hiyo mhandisi Nditiye ametoa Printer moja kwa shule ya sekondari ya Dokta Ally Mohamed Shein na kuahidi kutoa computer 25 zitakazogawanywa kwenye shule tano za sekondari zilizopo wilayani humo ambazo zitaunganishwa na internet ili zitumike kufundisha kwa njia ya masafa,msaada ambao umeahidiwa pia na mbunge Mtaturu.