Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:23 am

News: ''Serikali haijazuia kutoa rufaa ya matibabu nje ya nchi'' , Waziri Ummy.

DODOMA: Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema hakuna daktari aliyezuiliwa kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda nje ya nchi kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.

Ameeleza kwa sasa nchi ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutoa rufaa kwa wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.

Ummy ametoa kauli hiyo wakati akizindua mtambo maalum wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo uzibuaji wa mishipa ya moyo kwenye Hospitali ya Benjamini Mkapa, jijini hapa.

Amesema hadi sasa taifa limeweza kupunguza kupunguza idadi ya wagonjwa wa moyo waliokuwa wakitibiwa nje ya nchi kwa asilimia 95.

"Kwa mwaka 2017 Hospitali ya Jakaya Kikwete imewefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa wa moyo wenye kuhusisha upasuaji kwenye kifua 127 lakini kwa mwaka jana idadi hiyo imefikia wagonjwa 275 huku idadi ya wagonjwa 1025 walifanyiwa upasuaji wa moyo bila kufungua kifua.

“Nchi inauwezo wa kutoa huduma za matibabu kibingwa. Hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi," amefafanua.

Ameongeza serikali itaendelea kuboresha huduma za afya ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba kwa lengo la kuhakikisha kila kanda kunakuwepo na mtambo wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Amesema kuwepo kwa maabara hiyo kunaipunguzia mzigo wa wagonjwa Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI).

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk.Alphonce Chandika alisema kuanza kwa maabara hiyo kunaleta tabasamu kwa wanufaika kutokana na kuwepo na kazi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

“Tulidhamiria kuanzisha maabara hii kutokana na magonjwa yenyewe kwa kuwa na ongezeko kubwa ya moyo jambo linalohatarisha na kupoteza nguvu kazi ya Taifa,”alisema.

Dk.Chandika alisema Rais John Magufuli amekuja na sera ya kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati, kama kutakuwa na nguvu kazi yenye wagonjwa azma hiyo inaweza isitimie.

“Hivyo kuanzisha kwa huduma hii tunaenda kwenye nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati, jambo la kujivunia, takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO) zinaonesha kwamba takribani watu milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa ya moyo,”amesema.

Hata hivyo alisema kwa Tanzania bado hakujafanyika utafiti wa kina kubaini ukubwa wa matatizo ya ugonjwa wa moyo lakini takwimu za kwenye vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa wagonjwa wengi wanaofika wanagundulika na magonjwa hayo.

“Takwimu kutokana Chama cha Madaktari wa watoto(PAT) zinaonesha takribani watoto 13,600 wanazaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa ya aina mbalimbali ya moyo huku 3,400 kati yao wakihitaji kufanyiwa upasuaji,”alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwepo kwa maabara hiyo kutaokoa maisha ya watoto na watanzania wengi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Pamoja na hayo, amesema Hospitali hiyo imejipanga kuwa na maabara maalum ya upasuaji na tayari vifaa vimeshanunuliwa na kuna wataalam wanajifunza namna ya upasuaji wa moyo.

“Kwa kipindi cha miezi minne kutoka Septemba hadi Desemba 2018, wataalam wetu walihudumia wagonjwa wa moyo 942 kwa wingi huu unaonesha tatizo lilivyokubwa na linahitaji nguvu ya pamoja,”amesema.

Kadhalika, amesema hospitali ipo kwenye maandalizi ya kufunga mtambo wa kuvunja mawe kwenye figo ambapo utakuwa ni wa aina yake nchini.

“Kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha tuna matumaini makubwa mtambo utaanza kufanya kazi, tutahakikisha tunatangaza huduma hizi hata nje ya mipaka ya Tanzania ili ndege ziwe kujaa kwa kuleta wagonjwa kupata huduma,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohammed Janabi, amesema kwenye ukanda wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, Tanzania inaongoza kwa kutoa tiba ya maradhi ya moyo kwa wagonjwa wengi.

Amesema kwa mwaka jana wagonjwa 1056 walifanyiwa upasuaji wa maradhi hayo ambapo kati yao ni wagonjwa sita pekee waliofariki dunia.

Profesa huyo amesema wakiwa kwenye Hospitali ya Benjamini Mkapa, wameshawafanyia upasuaji wagonjwa 13.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainab Chaula, amesema madaktari wanafanyakazi ngumu ya kuhudumia Watanzania hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele.

Amesema ni muhimu kwa wataalamu hao kulindwa na kupewa nafasi ya kuwahudumia wananchi bila kunyanyaswa.