Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 10:59 am

NEWS: SEREKALI YATAJA MAFANIKIO YA MIAKA 4 YA RAIS MAGUFULI MADARAKANI

SERIKALI ya Tanznia imesema kuwa imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria inayohakikiwa kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuleta manufaa endelevu kwa faida ya Watanzania wote.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Vyombo vya Habari aliozungumzia kuhusiana na tathimini ya miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli.

Dkt. Abbasi alisema yapo mambo mengi na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali ya Awamu hivyo ili kuwezesha mafanikio yake yanaleta matokeo chanya kwa Watanzania na jamii kwa ujumla, Serikali imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria kwa ajili ya kulinda mafanikio hayo hata baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kumaliza muda wake.

‘‘Tanzania kwa sasa ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne ya Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano tumeweza kufanya mambo mengi ikiwemo suala la rushwa ambalo limekuwa kero kubwa kwa Watanzania na hilo kwa sasa tumeunda Mahakama maalum ya Mafisadi ambayo tayari imesikiliza kesi zaidi ya 50’’ alisema Dkt. Abbasi.

Aidha aliongeza zipo ahadi za utelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya Serikali iliyoahidiwa kufanywa na Rais Dkt. John Magufuli ambayo awali ilikuwa ikileta kero na kuchelewesha maendeleo ya Watanzania, ambapo ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano yameweza kutekelezwa.

Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi alisema ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutimiza ahadi mbalimbali ambazo tayari zimeanza kuleta matokeo chanya kwa Watanzania ikiwemo ununuzi wa ndege za Serikali ambapo awali jambo hilo lilikuwa na ugumu katika utekezaji wake.

‘Jambo jingine ni suala la kuhamia Dodoma, jambo hili kwa sasa si ndoto tena kwani kwa sasa asilimia 90 ya watumishi wa Serikali katika Wizara na baadhi ya Idara, Taasisi na Wakala za Serikali wamehamia Dodoma na Serikali imeweza msingi wa kisheria wa kuitangaza Dodoma kuwa ni makao makuu ya Serikali’’ alisema Dkt. Abbasi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema ili maendeleo hayo yazidi kuleta manufaa endelevu kwa vizazi vijavyo, Watanzania hawana budi kuwa wazalendo na kuwa walinzi wa mali za umma na kutoa taarifa katika mamlaka za serikali kuhusu uharibifu na ubadhirifu unaofanywa na mtu au kikundi chochote katika jamii.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali ya Awamu ya Tano kupitia ushirikiano wake na wananchi imeweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, maji, elimu na barabara, ambayo imeendelea kuwagusa wananchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini.

Akitolea mfano, Dkt. Abbasi alisema Serikali inatekeleza miradi ya maji 1600 nchi nzima ikiwemo miradi 300 inayotekelezwa katika maeneo ya vijijini na kutumia kiasi cha Tsh Bilioni 700 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo katika maeneo ya mijini ili kuhakikisha kuwa inafikia kiwango cha asilimia 85 vijijini na asilimia 95 maeneo ya mijini ifikapo mwaka 2020.

Kuhusu sekta ya afya, Dkt. Abbasi alisema Serikali kwa sasa imeendelea kuimarisha sekta hiyo kwani kwa sasa Tanzania imekuwa nchi mfadhili kwa kuweza kufanya huduma mbalimbali za kibingwa ambazo zilikuwa zikifanyika nje ya nchi na kuifanya Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha za Watanzania.

‘Ndani ya kipindi cha miaka minne Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka Tsh Bilioni 31 mwaka 2014/15 hadi kufikia Bilioni 270, na pia kuajiri waganga wataalamu zaidi ya 6000 wanaohudumia wagonjwa katika hospitali zetu za Mikoa, Wilaya, Vituo vya Afya katika Kata na Zahanati katika maeneo ya vijijini’’ alisema Dkt. Abbasi.