Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:27 am

NEWS: SEREKALI YAPOKEA MKOPO WA SH BILIONI 589.2 KUTOKA BENKI YA AFRIKA

Dar es Salaam: Serikali ya Tanzania imepokea mkopo wa Sh589.26 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kakonko Kasulu na Manyovu mkoani Kigoma yenye urefu wa kilomita 260.

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo ya uchumi wa viwanda na jamii kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa utilianaji wa saini wa mikataba hiyo leo Jumanne Machi 5, 2019 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema mradi huo utawaondolea adha ya usafiri ya muda mrefu wakazi wa Kigoma na kufungua milango ya maendeleo ya kiuchumi na kusaidia kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda wa nchi za Afrika Mashariki. "Barabara ya Kabingo-Kasulu na Manyovu ni kiunganishi muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi.”

“Mradi huu pia utakwenda sambamba na ujenzi wa Barabara ya Rumange -Gitazi yenye urefu wa kilomita tano nchini Burundi, yote hii ni kuboresha mtandao wa barabara za Afrika," amesema.

Amesema mbali na kuleta maendeleo ya kiuchumi pia utekelezaji wa mradi huo utapunguza adha ya usafiri na gharama za utengenezaji wa magari na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii. "Kwa muda mrefu Kigoma imekuwa nyuma kimaendeleo. Kupitia mradi huu tunaenda kuifungua Kigoma katika uchumi na maendeleo na ikumbukwe fedha hizi ni za mkopo wenye masharti nafuu ambao utalipwa ndani ya miaka 30 hadi 40," amesema.