Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 6:33 pm

NEWS: SEREKALI YAKANUSHA KUZUIA RIPOTI YA IMF JUU YA UCHUMI WA TANZANIA

Dodoma: Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa ripoti ya tathimini ya Uchumi wa Tanzania na Shirika la Fedha Duniani (IMF) bali inaendelea na mazungumzo na shirika hilo.

Kauli hiyo Waziri Mpango imetokana na swali la Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka leo, Aprili 23, 2019 ambaye kimsingi alitaka kujua ni kwa nini Tanzania imezuia uchapishaji wa taarifa IMF.

Mwakajoka aliibua hoja hiyo alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa baada ya IMF kuijuza dunia tangu Aprili 17 ilipotoa taarifa kuwa baada ya kikao chake, Serikali ya Tanzania, imezuia kuchapisha tathmini iliyofanywa wala kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Baada ya taarifa hiyo fupi, vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti na baadhi ya wanasiasa pamoja na wanaharakati kujitokeza wakitaka taarifa itolewe ili wananchi wajue mwenendo wa uchumi wao.

Baada ya kauli hiyo ya Waziri Dkt Mpanga, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) Zitto Kabwe aliahidi kutoa ripoti hiyo kwenye vyombo mbalimbali vya habari, na Kwenye mitandao ya habari.

"Kuna juhudi kubwa kwenye suala la Ripoti ya IMF Kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania. Jana wenzetu Chadema wameitaka Serikali iseme kitu, leo Waziri wa Fedha ‘kasema kitu’ Bungeni na kuna baadhi ya wanasiasa wanaongea na Press sasa hivi. Niliahidi kuweka Ripoti wazi LEO"

"Nimeona nifanye ifuatavyo 1) Nitawapa Ripoti hiyo Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni ndani ya muda mfupi ujao 2) Nitaiweka ONLINE ili watu wanaoihitaji waisome ( nitaomba tovuti zitakazokubali kuiweka waiweke) na 3) nitapost hapa Twitter vipande muhimu vya Ripoti hiyo" amesema Zitto