Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:38 pm

NEWS: SEREKALI YAKANUSHA KUNYIMWA MKOPO NA BANK YA DUNIA

Dodoma. Msemaji mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amekanusha uvumi kuhusu madai kuwa Benki ya Dunia (WB) imesitisha kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni za Kimarekani kwa kwa Serekali ya Tanzania, akisisitiza kuwa bado wapo kwenye mazungumzo na Benki hiyo.

Abbas ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 30, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Dk Abbasi ameeleza hayo baada ya kikao cha bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ambacho kingetoa uamuzi kuhusu kuruhusu mkopo huo kuripotiwa kuahirishwa.

Fedha za mkopo huo ambazo ni zaidi ya Sh1.2 Trilioni zingeelekezwa katika programu za shughuli za elimu.

Kikao hicho kilipangwa kufanyika Jumanne Januari 28, 2020 kwa ajili ya kuidhinisha mkopo huo, lakini kikaahirishwa dakika za mwisho kutokana na kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari vya nje kuwa ni ombi la taasisi ya kijamii ambayo ina wanachama wake Tanzania.

Katika maelezo yake leo, Dk Abbasi amesema, “walipanga kukutana siku fulani, mmoja wa wawakilishi wao aliomba wakutane leo, mtu anatoka hapo mishipa imekutoka eti mkopo umesitishwa, kukopa unaweza kuomba benki moja ukakosa nyingine ikakubali kwa hiyo ni majadiliano yanaendelea.”

“Huwezi kwenda tu ukasema unakopa halafu ukakubaliwa lazima majadiliano yafanyike.”

Msemaji huyo wa Serikali alijibu madai ya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kuwa Tanzania imenyimwa mkopo huo kwa madai kuwa fedha hizo zitatumika katika uchaguzi mkuu badala ya elimu.

“Tulifanya uchaguzi wa Serikali za mitaa, chaguzi za marudio na sasa tume za uchaguzi zinafanya vikao kwa ajili ya uchaguzi, sasa fedha hizo zinatoka Benki ya Dunia? Dunia haiwezi kuamini maeneo yake (Zitto). Dunia ina akili, ina macho” amesema Dk Abbasi.