Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:50 am

NEWS: SEREKALI YA KENYA YAONDOA MARUFUKU YA KUTEMBEA USIKU

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020. Kenyatta ametangaza hilo alipoiongoza nchi yake kuadhimisha siku ya Mashujaa hii leo Octoba 20, 2021.

Rais Kenyatta ameiongoza Kenya kuadhimisha siku ya mashujaa huku akitangaza kwamba ameondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020. Sherehe hiyo iliyofanyikia katika jimbo la Kirinyaga, ilihudhuriwa na rais wa Malawi Lazurus Chakwera na viongozi wa upinzani nchini humo.

Wakenya wa matabaka mbali mbali walivumilia mvua na kibaridi kikali katika uwanja wa Wang'uru, ulioko katika jimbo la Kirinyaga, na kuhudhuria sherehe ya 58 ya mashujaa awali ikijulikana kuwa siku ya Kenyatta. Ni sherehe ambayo huwakumbuka waasisi wa taifa hilo waliopigana kumtimua beberu pamoja na wakenya waliofaulu katika Nyanja mbali mbali.

Akilihutubia taifa, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa, serikali yake imeweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Tamko lake likijiri wakati ambapo uchumi wa kenya ukiyumba kutokana na marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwa ikizingatiwa kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri. Kufungwa uchumi wa taifa ambao ulikuwa umefungwa kwa kipindi kirefu kumekuwa na athari hasi kwa Wakenya wengi.