Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:54 pm

NEWS: SASA NI RUKSA KUMSHTAKI RAIS WA TANZANIA

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam imetupilia mbali mapingamizi sita yaliyowasilishwa na mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) kupinga usikilizwaji wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kiongozi Mkuu wa chama cha (ACT Wazalendo ), Zitto Kabwe dhidi ya uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.


Zitto kupitia kwa wakili wake Nyaronyo Kicheere anamshtaki Rais wa Tanzania John Magufuki kwa kumuondoa kimakosa kwa aliyekuwa CAG, Profesa Mussa Assad kabla ya kufikisha miaka 65 ya kustaafu kama Katiba inavyotamka.

Hoja zingine ni kupinga Rais kumteua Kichere kabla ya Profesa Assad kumaliza muda wake; mwanasheria mkuu (AG) kwa kumshauri vibaya Rais; na Profesa Assad. Pia, wanaiomba Mahakama Kuu kutamka kwamba Kichere siyo CAG na imtamke Profesa Assad ni CAG halali.

Hata hivyo, AG aliweka mapingamizi sita kupinga kesi hiyo ya kikatiba akidai maombi yaliyowasilishwa na Zitto yana kasaro, hayana nia nzuri na yanakinzana na sheria.

AG alidai maombi hayo yana makosa kwa kuwa yameletwa dhidi Rais wa Tanzania siyo sahihi, hati ya kiapo iliyounga mkono maombi hayo ina kasoro.

Pingamizi lingine ni kupinga njia iliyotumika ambapo sio sahihi kwa maombi hayo kuwasilishwa.

Akijibu hoja hizo, wakili Kicheere alidai kuwa Katiba inaruhusu Rais kushtakiwa kwa mambo aliyoyafanya kama Rais ila hawezi kushtakiwa binafsi na kwamba, utaratibu waliotumika kuwasilisha kesi hiyo ni sahihi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha baada ya kupitia hoja za pande zote zilizowasilishwa kwa maandishi, alitupilia mbali mapingamizi ya AG.

Jaji Mlacha alisema wajibu maombi (Serikali) waliwasilisha mapingamizi hayo kwa maandishi na waleta maombi wakajibu kwa maandishi kwa muda uliopangwa kisheria.

“Baada ya kupitia hoja zote nimejiridhisha kuwa mapingamizi yote yaliyowasilishwa hayana mashiko hivyo nayatupilia mbali,” alisema.

Baada ya kutupa mapingamizi hayo, mahakama hiyo ilipanga kuanza kusikiliza shauri hilo Aprili 14 mbele ya jopo la majaji watatu; Mlacha, Benhaji Masoud na Juliana Masabo.