- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: SALIM AHMED SALIM APONGEZWA KUPOKEA TUZO YA HESHIMA
Dar es Salaam. Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amempongeza Waziri Mkuu Mstaafu Dk Salim Ahmed Salim kwa kupewa nishani ya juu ya urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China, huku pia akiwataka Watanzania kutekeleza majukumu ya kitaifa wanayopewa kwa uzalendo usiotiliwa shaka,uaminifu na ufanisi.
Kutokana na tuzo hiyo, Dk Salim anakuwa Mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki leo Septemba 29 imesema Waziri Kabudi amesema tuzo hiyo imeliletea heshima Tanzania na yeye mwenyewe kutokana na utendaji wake usiotiliwa shaka baada ya kukabidhiwa majukumu hayo na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Amesema Dk Salim ni Mtumishi mwaminifu na mzalendo kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi katika nafasi mbalimbali alizofanya kazi ambazo ni pamoja na ukurugenzi katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki balozi katika nchi za Misri, India, China na Umoja wa Mataifa.
Nyingine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mambo ya Nje, Naibu Waziri Mkuu kisha Waziri Mkuu na baadae Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Nishani hiyo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping ilipokelewa na Maryam Salim, Binti wa Dk Salim ambaye pia ni mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya.
Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki.
Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Wang Qishan, Waziri Mkuu Li Keqiang, Spika wa Bunge Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa.
Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China imetolewa kwa Dk Salim kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.