Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:29 am

NEWS: SAKATA LA EPA MWEZI UJAO

HATIMA ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA) baina ya nchi hizo na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU), sasa inatarajiwa kujulikana mwezi ujao wakati wa kikao cha wakuu wa nchi za EAC.

Mwenyekiti wa EAC ambaye pia ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekaririwa akiyasema hayo mara baada ya kikao chake na Rais wa Tume ya Ulaya, Jean-Claude Juncker wiki iliyopita. Aliwasilisha mawazo ya nchi wanachama ikiwemo Tanzania iliyoonesha kutokuwa tayari kusaini mkataba huo kwa kuwa unaonekana kutokuwa na maslahi kwa nchi za EAC. Mkutano huo ulilenga kujadili nafasi ya kiuchumi ya EAC na pia kutoiadhibu Kenya kutokana na nchi wanachama kutosaini mkataba huo. “Niliwasili Ubelgiji kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Kama Mwenyekiti wa EAC, nimewasilisha hoja za wanachama kuhusu EPA,”Rais Museveni amekaririwa kupitia mtandao wake wa Twitter. Aliongozana na Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumukeko, mawaziri wa biashara kutoka nchi wanachama, huku nyingine zikiwakilishwa na manaibu waziri na makatibu wakuu wa wizara. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Kenya, Betty Maina alisema Rais Museveni aliwasilisha hoja zake kwa ufasaha ikiwa ni sababu za Tanzania kusita kuridhia kusainiwa kwa mkataba huo, hivyo kuomba ufafanuzi wa EU.

“Tunatarajiwa kabla ya Novemba mwaka huu EU itatoa ufafanuzi, na hivyo uamuzi wa nchi wanachama wa EAC utajulikana Novemba,” alisema Maina. Msimamo wa Tanzania Mapema mwaka huu, Rais Magufuli na Museveni walikutana jijini Dar es Salaam na kukubaliana kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli alibainisha kuwa mazungumzo yao pia yalilenga suala la kusaini mkataba wa EPA ambapo alisisitiza Tanzania haitasaini mkataba huo akibainisha kuwa hiyo ni njia nyingine ya ukoloni. Alisema: “Tumezungumza kwa kina na Rais Museveni na tumekubaliana kuendelea kulizungumza. Nimemueleza kuwa sisi Tanzania tunaona EPA haina faida na ni ukoloni mwingine, ambao unaletwa kwa sababu ya mambo mengi.

“Hatuwezi kuzungumzia kujenga viwanda wakati huo huo tunashindana na watu wenye viwanda vikubwa… Na yeye Rais Museveni amesema kimsingi anapenda kufanya kitu chenye faida.” Kwa upande wake, Rais Museveni alisema kutokana na msimamo wa Tanzania katika suala la EPA, ameamua kuja kufanya mazangumzo na Rais Magufuli ili kuwa na msimamo wa pamoja.

Na hata viongozi wa EAC walipokutana katika mkutano wa 18, akizungumza katika mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi za EAC mara baada ya kukabidhiwa kijiti cha kuiongoza jumuiya hiyo na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam, Mei mwaka huu, Rais Museveni alisema, bado kuna mambo yaliyomo katika mkataba huo yanahitaji ufafanuzi na kuhoji jumuiya hiyo itawezaje kusaini mkataba huo hali ya kuwa mwanachama wao amewekewa vikwazo na Umoja huo wa Ulaya.

“Tutawezaje kujadili na kusaini mkataba hali ya kuwa mwanachama wetu mmoja amewekewa vikwazo na EU? Bado tunahitaji ufafanuzi juu ya mambo kadhaa yaliyomo kwenye mkataba wa EPA,” alisema Museveni. Aidha, Rais Museveni alieleza kutofurahishwa na hatua ya Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Burundi bila kushauriana na viongozi wa jumuiya hiyo.

Alisema Burundi ni tatizo la jumuiya hiyo, hivyo wanaweza kulimaza wenyewe. Tayari nchi za Kenya na Rwanda zimeshasaini mkataba huo, lakini ziko katika hatari ya kupoteza masoko yake ya nje katika nchi za Ulaya kutokana na kuonekana kama nchi zinazoendelea huku nchi nyingine za jumuiya hiyo zikioneokana kuwa chini. Kutokana na nchi za Afrika Mashariki kuwa na Himaya Moja ya Forodha, ni lazima nchi nyingine ambazo ni Tanzania, Burundi, Uganda na Sudan Kusini zisaini mkataba huo ili uweze kutekelezeka.

Awali, Dk Magufuli alisema jambo hilo ni changamoto, kwani ameshindwa kulimaliza kwa wakati wake, lakini anaamini chini ya Rais Museveni litaweza kufikiwa mwafaka. “Wakati tunaambiwa kusaini, Umoja huo huo umeiwekea vikwazo Burundi ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini wao kule wameshagombana wameacha, Uingereza imeshajitoa, kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kwa sisi kuamua,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ana uhakika chini ya Uenyekiti wa Rais Museveni atapambana na changamoto hiyo na kufikia mwafaka na kwamba yeye ameshindwa kulimaliza na hasa kwa sababu ya masharti yaliyomo kwenye mkataba huo. Alisema masuala hayo watayazungumza na Umoja wa Ulaya juu ya kuangalia masuala yanayofanya Jumuiya hiyo ishindwe kusaini na kuangalia mwafaka wa Burundi ni mwanachama wa EAC, hivyo wakiondoa vikwazo juu ya nchi hiyo itasaidia kusaini mkataba huo.