Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:53 am

NEWS: RC GAMBO AJUTIA KUWASWEKA WATUMISHI RUMANDE SAA 24

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha nchini Tanzania (RC), Mrisho Gambo amesema anajutia vikali hatua alizokuwa anawachukila za kuwaweka rumande saa 24 watumishi wa umma waliokuwa wanafanya makosa mbalimbali bila kuwasikiliza.

Simulizi ya Majuto hayo ameyatoa Leo Jumapili Novemba 24, 2019 kupitia ukurasa wake wa Instagram na kusema watu wasione siku hizi hawaweki watumishi ndani wakadhani hana mamlaka hapana kwani ametambua kuwa elimu haina mwisho na amekubali kujifunza.Image result for rc mrisho gambo ofisini"

''Usione siku hizi siweki watumishi ndani ukadhani sina Mamlaka, siku hizi mamlaka ni Makubwa zaidi kuliko siku za nyuma lakini nimetambua kuwa Elimu haina mwisho na nimekubali kujifunza Uongozi.''

"Nimeamua kujikosoa pamoja na kufanyia kazi maoni ya wanaonikosoa, sisi viongozi vijana bado ni wanafunzi wa uongozi, kila siku tunajifunza na kupata uzoefu, hakika uzoefu ni mwalimu mzuri," amesema Gambo

Gambo katika kueleza kujutia kwake alitoa uzoefu wake kwa matukio kadhaa ambayo yaliyomfanya ajutie swala la kuwaweka ndani watumishi wa umma bila kuwasikiliza

"Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma mwaka 2015/2016 nilielekeza Mkurugenzi aniandalie kikao cha haraka cha watendaji wa kata na vijiji. Kwenye kikao hicho mtendaji wa kata ya Itebula alichelewa kufika kikaoni na bila ya kumsikiliza nikaelekeza awekwe ndani kwa saa 24.
Kama ilivyo kawaida kesho yake nikaagiza aletwe ofisini kwangu kwa ajili ya utetezi.

Image result for rc mrisho gambo ofisini"

Mtumishi yule alipofika ofisini akaanza kujitetea kwa kuniambia “ Mkuu, wakati napata wito wa kikao chako nilikuwa hospitali na Mke wangu. Mke wangu ni mjamzito na alipata matatizo ya Mimba, muda ule napata wito alikuwa chumba cha upasuaji. Kwa kuheshimu wito wako Mkuu nilimwacha mke wangu hospital nikakimbia kuja kwako. Nilidhani nikifika utanipa pole na kuona nimeheshimu wito wako, badala yake ukaniweka ndani.

Leo nimepata taarifa kuwa hali ya Mke wangu na mtoto aliyeko tumboni ni mbaya zaidi. Mkuu, tukio hili sitalisahau kwenye maisha yangu na mimi nadhani ulininyanyasa na kunionea kwasababu ya unyonge wangu. Hakika hapa umetumia ubabe na madaraka yako vibaya”.

Kwa hakika nilitamani kulia. Nilijisikia vibaya sana. Nilimuomba radhi mtumishi huyu ikiwa ni pamoja na kumrudishia nauli pamoja na mwenzie wa kijiji cha Sibwesa kata ya Kalya." amesimulia Gambo

Tukio la 2. "Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma mwaka 2015/2016, siku moja nilimuagiza Mkurugenzi aniandalie kikao cha ghafla cha watendaji wa vijiji na kata. Kwenye kikao kile watendaji wawili walichelewa kwa zaidi ya masaa 5 nikaagiza wawekwe ndani masaa 24.
Baada ya saa 24 nikaelekeza waletwe ofisini ili nipate utetezi wao.

Mmoja alikuwa ni mtendaji wa Kijiji cha Sibwesa kwenye kata ya Kalya ambako ni Kilomita 422 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Uvinza eneo la Lugufu. Mtendaji kwenye maelezo yake aliniambia“ Mkuu nakiri kupokea wito wako wa dharura lakini kwa masaa 6 nisingeweza kuwahi kutokana na umbali wa Km 422 kutoka kijiji kwangu na makao makuu. Kutoka kijijini kwangu ambako ni Barabara ya vumbi lazima nipande pikipiki umbali wa Km kama 30 hivi, halafu nipande Boti kisha nipande basi ndio nipate hiace ya kufika Wilayani.

Kwa hakika hata sikupewa nauli na gharama si chini ya laki moja ambayo ni karibu nusu ya mshahara wangu. Lakini kwasababu ya wito wa Mkuu nilitumia gharama zangu binafsi na kukimbazana ili niwe nimetii maagizo yako.

Cha kusikitisha nilipofika tu hata kabla ya kunisikiliza ukaagiza niwekwe ndani saa 24. Akaniambia Mkuu mimi nadhani pale ulinionea na ulitumia mamlaka yako vibaya”. Kisa hiki cha kweli kilinifanya niache mchezo wa kuwaweka ndani watumishi. Nikaona haja ya kuwasikiliza watumishi kabla ya kuwahukumu.


"Watumishi wetu ni binadamu. Wana changamoto nyingi kama binadamu wengine. Busara ni kuwapa fursa ya kujitetea kabla ya kuwahukumu. Hekima ni kushughulikia changamoto zao kwa kufuata kanuni za utumishi wa Umma. Kupitia kanuni za Utumishi watapata wasaa wa kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.