Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 12:51 am

NEWS: RAIS WA MISRI ATUA LEO

DAR ES SALAAM: RAIS Abdel Fattah Al Sisi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri amewasili nchini leo kwa ziara ya kitaifa Tanzania kwa mwaliko wa Rais John Magufuli.

Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Rais Al Sisi nchini Tanzania tangu Dk Magufuli aingie madarakani Oktoba mwaka 2015. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, lengo la ziara ya Rais Al Sisi ni kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili, na itatoa fursa kwa viongozi hao kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa.

Ratiba iliyopatikana jana jioni inaonesha kuwa Rais Al Sisi atawasili leo mchana na kupokelewa na mwenyeji wake, Dk Magufuli, na baadaye kuwa na mazungumzo (tete-a-tete) na mwenyeji wake kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi na baadaye jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake. Rais Abdel Fattah Al-Sisi alizaliwa Novemba 19, 1954 jijini Cairo na ni rais wa sita wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri tangu mwaka 2014.

Taarifa hiyo ya wizara iliyotolewa mwishoni mwa wiki, ilieleza kuwa Tanzania na Misri zina mahusiano mazuri ya kidiplomasia ya muda mrefu ambayo yamezidi kuimarika hasa katika miaka ya karibuni. Ushirikiano huu unatokana na misingi ya mahusiano na mashirikiano ya karibu sana kati ya Baba wa Taifa na muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Kiongozi mashuhuri wa Misri na muasisi wa Jamhuri ya Taifa la Kiarabu ya Misri, Gamal Abdel Nasser.

“Uhusiano wa nchi hizi mbili umejengwa katika misingi ya ushirikiano na maelewano katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama pamoja na medani za siasa za ushirikiano kimataifa, kutetea haki za binadamu, kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika, ukombozi wa Bara la Afrika na kupinga ukoloni, dhuluma na aina zote za ukandamamizaji duniani.

“Uhusiano huu umejengwa katika nyanja zote za uhusiano katika sekta za huduma za kijamii na kiuchumi zikiwemo elimu, afya, kilimo, mawasiliano, usafiri, ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa,” ilifafanua taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Misri ni nchi ya pili yenye uchumi mkubwa barani Afrika. Takwimu za mwaka 2016, zinaonesha kwamba Pato la Taifa (GDP) la Misri lilikuwa Dola za Marekani bilioni 266.213.

Sekta kubwa katika uchumi wa Misri ni sekta ya huduma (huduma za benki, mawasiliano, usafirishaji na utalii) ambayo inachangia takribani asilimia 52.5 kwenye GDP. Viwanda inachangia asilimia 36.3, na kilimo asilimia 11.2. Aidha, Tanzania na Misri zinashirikiana katika ngazi za taasisi za serikali ambazo ni Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri ambayo inashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Tanzania (Takukuru) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar zimesaini makubaliano ya Ushirikiano na Hospitali ya El Shatby ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri.

Pia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina ushirikiano wa kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa Shahada za Juu za Uzamili na Uzamivu na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA JKT wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya Polyserve ya Misri.

Pia kutokana na takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili jumla ya miradi minane kati ya mwaka 1990 hadi 2017, miradi hiyo ina jumla ya thamani ya Dola za Marekani 887.02 na kutoa ajira zipatazo 953, uwekezaji huo ni katika maeneo ya kilimo, viwanda (mbao, mbolea, madini, dhahabu na shaba) na sekta ya huduma. “Hivyo ziara hii ina umuhimu mkubwa sana hasa katika wakati huu ambapo msisitizo wa Serikali ni katika kujenga uchumi wa viwanda,” iliongeza taarifa ya wizara.

#Habarileo