Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:56 pm

NEWS: RAIS WA BURUNDI KULIPWA MABILIONI YA PESA

Wabunge nchini Burundi juma hili wamepitisha muswada wa sheria ambao utampa kitita kikubwa cha fedha rais anayemaliza muda wake Pierre Nkurunziza ikiwemo nyumba ya kifahari na karibu Dola za Marekani 500,000.

Hatua ya bunge imekuja ikiwa imesalia miezi minne tu kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi Mei ambapo rais Nkurunziza amesema hatogombea.

Mswada huo wa sheria unaeleza kuwa katika kila kipindi cha miaka 7, baada ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia kumaliza muhula wake, mbali na marupurupu hayo, kiongozi anayemaliza muhula wake atakuwa na mshahara na faida zingine sawa na makamu wa rais ambaye yuko madarakani.

Waziri wa sheria Aime Laurentine Kanyana, amesema sheria ni vema rais anayemaliza muda wake kuheshimiwa na kukipa heshima kiti cha urais nchini humo.

"Inapendeza kuona rais anayeondoka madarakani akipewa heshima, hili tunafanya kwa raia huyu, wale wanaokuja, na wale waliopita," alisema bungeni.


Hata hivyo, Agathon Rwasa mwanasiasa wa upinzani anakosoa hatua hiyo ya kutoa kiwango kikubwa cha fedha kwa rais anayeondoka madarakani na kusema lengo ni kumliwaza rais Nkurunziza ili asipate hamu ya kutaka kuwania tena.

"Pengine chama chake kimeona kuwa watumie njia hii ili asitamani kurejea madarakani ili asigombee tena, ila kwa hali ya uchumi wa nchi inashtua kidogo kuhusu kiasi hicho, " aliongeza.

Mswada huu pia unaeleza kuwa rais anayeondoka madarakani atakuwa na kinga ya kutoshtakiwa.