Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 2:39 am

NEWS: RAIS TRUMP AMTAKA RAIS WA CHINA KUTATUA MZOZO WA HONG KONG

Rais Donald Trump wa Marekani ameihimiza China kutumia njia za kiutu kusuluhisha mgogoro wa waandamanaji wanaotaka demokrasia mjini Hong Kong, huku kukiwa na wasiwasi kwamba China inafikiria kuuingilia moja kwa moja mgogoro huo.

Handelskonflikt China-USA (picture-alliance/dpa/S. Walsh)

Picha zilizochukuliwa na shirika la habari la AFP zilionesha maelfu ya wanajeshi wa China wakipeperusha bendera nyekundu wakiwa katika uwanja wa mchezo mjini Shenzhen mpakani mwa mji wa Hong Kong.

Magari kadhaa ya kivita pia yalikuwa yameegeshwa karibu na eneo hilo. Kukusanyika kwa wanajeshi hao kunakuja wakati rais wa Marekani alipounganisha uwezekano wa makubaliano ya biashara na China na suluhu ya amani ya mgogoro wa kisiasa mjini Hong Kong unaoendelea kwa zaidi ya wiki kumi sasa.

Marekani ina wasiwasi juu ya maafisa wa usalama kukusanyika mpakani mwa Hong Kong, huku maandamano yakizidi kupamba moto na China nayo ikiendelea kulitisha vuguvugu linalodai mabadiliko ya kidemokrasia.

Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Twitter, Trump alipendekeza mkutano na Rais Xi Jinping wa China kusaidia kuutatua mzozo huo. Katika ujumbe huo, Trump ameongeza kuwa kama China inataka kuingia katika makubaliano, itabidi kwanza ishirikiane na Hong Kong kwa njia ya kibinadamu na kwamba hana hofu kuwa Rais Xi anataka kutatua mzozo huo mara moja kwa njia za kiutu.

Trump, ambaye amekuwa akitafuta mkataba mkubwa na kurekebisha ukosefu wa usawa wa kibiashara na China kabla ya kampeni yake ya kuwania muhula wa pili wa urais mwakani, amekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa bunge la nchi hiyo kwa kutochukuwa hatua thabiti kuhusiana na suala la Hong Kong na kutaja maandamano hayo mwanzoni mwa mwezi huu kuwa ghasia ambazo ni suala linalopaswa kushughulikiwa na China.

Wanaharakati bado wanapanga misururu ya maandamano makubwa mwishoni mwa juma hili katika juhudi za kuendeleza azma yao inayoungwa mkono na umma, licha ya ghasia zilizoshuhudiwa wiki hii walipopiga kambi katika uwanja wa ndege wa eneo hilo na kutatiza shughuli za kawaida.