Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:21 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI '' SASA NIMESHACHOKA MANENO TU"

Dar es salaam: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana Jumamosi tarehe 16 Machi, 2019 amewatimua wakala wa majingo Tanzania (TBA) kuendelea na Ujenzi wa Nyumba za makazi ya Askari Magereza wa gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ujenzi huo na kuagiza mradi huo ukabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

"Nimemuona Naibu Waziri wa Mambo ya ndani hapa anasema katibu mkuu wa wizara ya Ujenzi wakutane, wameshakutana? Si ametoa maagizo zaidi ya siku Nne tu, wameshakutana hapa, ni maneno tu, sasa nimeshachoka maneno tu. Sasa nimechoka maneno Kanali simamia hii kazi, panga wewe umalize, jeshi halishindwi" alisema Rais Magufuli

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kubaini kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya Serikali kutoa shilingi Bilioni 10 za ujenzi.

Ametaka wataalamu wa TBA waliokuwa wakisimamia mradi huo pamoja na Askari Magereza waondoke na kuwapisha JWTZ.

“Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA, nisimuone mtu wa Magereza kuja kusimamia, muwaache Jeshi la Wananchi wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi Magereza, kwa hiyo watu wa TBA kuanzia leo nimewafukuza hapa” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika mradio huo ambao ulianza zaidi ya miaka 2 iliyopita kwa kushirikisha Jeshi la Magereza ambalo lilikuwa linaisadia TBA katika kazi za ujenzi, na ametaka TBA na Jeshi la Magereza wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Nataka kila mlipo watu wa Magereza mfanye kazi, msimamie watu, kama ni ng’ombe muwafuge vizuri wazalishe vizuri hadi muuze mazao nje, kama ni kilimo mlime kwelikweli, muwe ni jeshi la kuzalisha, hii ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofari, tuanze kujenga”amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Charles Mbuge amesema JKT itakamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha miezi 2 na nusu kuanzia kesho na kwamba kazi zitafanywa usiku na mchana.