Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:51 am

NEWS: RAIS MAGUFULI AZIPA SIKU 60 TAASISI ZA SEREKALI KUTOA GAWIO

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa mashirika, na taasisi za Serekali zipatazo 187 kutoa gawio haraka kwa Serikali ndani ya miezi miwili sawa na siku 60 na amesema wakishindwa kufanya hivyo waondoke wenyewe kwenye nafasi zao.

Tamko hilo Rais Magufuli amelitoa leo Jumapili Novemba 24, 2019 Ikulu jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwenye taasisi, mashirika na kampuni ambazo serikali inamiliki au ina hisa zake.

Amesema Serikali ya Tanzania imewekeza mtaji wa Sh56 trilioni katika taasisi na mashirika 266, hata hivyo ameshangaa kuona ni mashirika 79 pekee ndiyo yametoa gawio kwa mwaka 2018/19 huku mashirika 187 yakishindwa kufanya hivyo. “Baada ya siku 60, bodi za mashirika hayo 187 ambazo zitakuwa hazijaleta gawio zijivunje zenyewe, waandike barua na kama ni wa kuteuliwa na mimi maana yake siku hiyo siyo mwenyekiti tena, kama wameteuliwa na mamlaka nyingine wazivunje hizo bodi,” amesema Rais Magufuli.

Rais amesema kuwa haiwezekani kila mwaka shirika linajiendesha kwa hasara wakati lina mwenyekiti wa bodi na watendaji wakuu wa mashirika hayo ambao wanalipwa mishahara mikubwa.

Amesema miezi miwili ikifika hataki kuona kiongozi yoyote ambaye hajapeleka gawio anabaki kwenye shirika. “Hatuwezi kuendelea kukaa na mashirika ya namna hii, hatuwezi kuendelea kukaa na viongozi wa namna hii, hatuwezi kuendelea kukaa na bodi za namna hii, ambazo tunazungumza lakini hawataki kuelewa,” amesema Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwaandikia barua viongozi wa mashirika na taasisi hizo ambazo hazijatoa gawio na kusimamia agizo lake la kuhakikisha kwamba asiyetoa gawio aondoke.