Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:16 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI AWANYOOSHEA KIDOLE WATENDAJI TANESCO RUKWA

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa tahadhari kwa baadhi ya watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa wanacheza mchezo mchafu.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 8, 2019 wakati akizungumza na wananchi akiwa njiani kwenda Kanazi Wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa kuzindua barabara ya Sumbawanga- Kanazi yenye urefu wa kilomita 75.

Akiwa njiani kuelekea katika eneo hilo, Rais Magufuli alisimama katika vijiji mbalimbali akizungumza na wananchi na kusikiliza kero zao zinazotolewa na viongozi wa maeneo hayo. Baadhi ya changamoto zilizotajwa kwenye vijiji alivyosimama ni umeme, maji na barabara.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alianza kujibu baadhi ya changamoto moja kwa moja na nyingine kuwaita mawaziri alioongozana nao, akiwataka kujibu.

Akijibu changamoto ya umeme, Rais aliwaambia wananchi kuwa Serikali inatarajia kumaliza changamoto ya umeme kwa kila kijiji kupitia awamu ya tatu ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (Rea) na kuwasisitiza wananchi kuendelea kujenga nyumba.

“Nia ya Serikali yangu ni kuleta maendeleo kwa kila mmoja, nataka watu watajirike ukipata hela yako jenga na mimi hapa nimefurahi kila mahali pamejengwa.” “Na umeme nataka niwahakikishie kila mmoja atapata, nawaambia ukweli najua kuna matatizo ya makandarasi na kuna mchezo mbaya unachezwa na baadhi ya watendaji wa Tanesco, watanikoma siku moja wataona,” amesema Rais Magufuli bila kuweka wazi mchezo unaochezwa na watendaji hao