Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:32 am

NEWS: RAIS MAGUFULI AONESHA MASIKITIKO MAKUBWA AJALI YA MOROGORO

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa watu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ya gari la mafuta iliyosababisha kulipuka kwa moto na kuteketeza watu zaidi ya 60 katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro.

Rais Magufuli ameitaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa pamoja kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa maisha yao.

Rais Magufuli ametuma salamu hizo leo Jumamosi Agosti 10, ambapo amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 62 na majeruhi 70.

“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote, ninawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wapone mapema,” amesema.

Aidha ameonesha kusikitishwa na kitendo cha watu wanaokimbilia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa zilizobebwa na magari hayo ambapo ametaka vitendo hivyo vikome.

“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanayobeba kemikali za sumu, yapo magari yanayobeba milipuko nakadhalika nawaomba sana tuache tabia hii,” amesema.

Lori lililokuwa limebeba mafuta aina ya petroli likitokea Dar es Salaam limepinduka na kuwaka moto katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro leo Jumamosi Agosti 10, ambapo takribani watu 57 wamepoteza maisha.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, amesema walipokea taarifa ya kuanguka kwa gari iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam lakini uelekeo wake haukufahamika ambalo lilianguka upande wa kushoto wa barabara likielekea uelekeo wa Dodoma, Iringa na baada ya kupinduka mafuta yalianza kumwagika.

“Watu wanaofanya shughuli katika eneo hili walianza kumiminika kwaajili ya kuchota mafuta ambayo yalikuwa yanamiminika kwa kasi kubwa lakini gafla ukajitokeza moto mkubwa ambao umesababisha watu takribani 57 kupoteza maisha lakini bado tunaendelea kufuatilia idadi kamili na miili hiyo kwa sasa iko hospitali huku ufuatiliaji ukiendelea ili kuwabaini majina yao,” amesema.

“Pia katika eneo hili tumekuta pikipiki zaidi ya 10 zikiwa zimeungua vibaya, bado tunafanya uchunguzi kujua zilikuja kufanya nini katika eneo hili tunadhani ni hao ambao walikuja kuchukua mafuta na zenyewe tunafanya utaratibu wa kuziondoka katika eneo hili,” amesema.