Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:26 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI AFUTA MBIO ZA MWENGE

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametangaza kufuta mbio za Mwenge za mwaka 2020 kwa ajili ya kuchukua tahadhari juu ya kuenea kwa ugonjwa wa corona.


Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu eneo la Ubungo linalounganisha barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela.


“Nina fahamu kitu kingine kinacholeta mkusanyiko ni mwenge na tulitegemea kuwasha mwenge karibuni kule Zanzibar ambapo ungewezwa kutembezwa nchi nzima, nimeamua mbio za mwenge hazitafanyika mpaka corona iwe imeondoka” amesema Magufuli.

Ugonjwa wa Covid - 19 umesababisha vifo vya zaidi ya watu 6,513 katika nchi mbalimbali Duniani na Zaidi ya watu karibu 150,000 wameambukizwa Ugonjwa huo na Sasa unataarifiwa kuwa umeshaingia katika nchi za Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Rwanda.

Rais Magufuli amesema fedha za mwenge ambao ulitakiwa kuwashwa Zanzibar zitatumika katika kujiandaa na tahadhari zaidi ya corona ambayo ishafika Kenya na Rwanda.


“Ndugu zangu ugonjwa huu unaua, watanzania tuchukue tahadhari, ugonjwa ushafika kwa majirani zetu ni lazima Watanzania tuchukue tahadhari utatumaliza” amesema Magufuli.


Magufuli amesema hadi sasa hakuna mgonjwa wa corona Tanzania na mbio za mwenge zitaendelea itakapothibitishwa ugonjwa huo umeisha duniani.
Magufuli ameendelea na ziara katika barabara zinazopanuliwa za Mwenge, Mbezi na Kimara kusisitiza wananchi kuchukua tahadhali za kutokugusana na kuepuka misongamano.


Rais Magufuli aliulizia kuhusu ujenzi wa soko la wamachinga eneo la Mbezi mwisho ambalo aliagiza lijengwe na hakukuwa na hatua iliyochukuliwa aliomba wananchi wampe muda ili afuatilie baada ya kupita muda mrefu bila hatua yoyote.
Mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo linalounganisha barabara ya Morogoro, Mandera na Sam Nujoma umefikia zaidi ya asilimia 70.


Katika maelezo yake Mfugale alimuonyesha Rais Magufuli katika mchoro wa ujenzi wa daraja hilo eneo jipya ambalo kutajengwa ghala la magari yaendayo haraka ambalo kwa sasa lipo Jangwani.
Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo unatumia zaidi ya Sh200 bilioni.


Rais Magufuli amepongeza ujenzi wa daraja hilo na kulidhika na maendeleo ya ujenzi huo na kuwapongeza wizara, Tanroads na wakandarasi.


“Tulipita daraja la Mfugale pale Tazara lile ni cha mtoto," amesema Magufuli.
Magufuli amesema wakati anasema jengo la Tanesco libomolewe kwakuwa lipo eneo la barabara walimuona kichaa ila sasa wanajionea.