Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:45 am

NEWS: RAIS MADURO YUPO TAYARI KUONGEA NA UPINZANI

Rais wa Venezuela Bw. Nicolas Maduro amesema yuko tayari kwa mazungumzo na upinzani na kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge wakati ambapo mpinzani wake Guaido amechachamaa kuitisha maandamano zaidi

Mapambano ya kuwania madaraka ya kuidhibiti Venezuela yamepamba moto baada ya serikali hii leo kushinikiza uchunguzi ambao huenda ukasababisha kukamatwa kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa mpito nchini humo Juan Guaido ambaye wakati huohuo ameitisha upya maandamano mengine.

Mahakama ya juu kabisa ya Venezuela imepitisha vikwazo dhidi ya Guaido kusafiri nje ya nchi hiyo na akaunti zake kuzuiliwa. Hatua hii inaonekana pengine inalenga kulipitiza kisasi kutokana na vikwazo ilivyowekewa Venezuela na Marekani katika biashara yake ya Mafuta.Vikwazo hivyo hapana shaka vinatarajiwa kuutikisa kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi hiyo mwanachama wa shirika la nchi zenye kuzalishwa kiwango kikubwa cha mafuta duniani OPEC,uchumi ambao tayari umeshaporomoka.

Guaido anatambuliwa kama rais na Marekani pamoja na nchi nyingi za Magharibi huku akionekana kuupa changamoto kubwa utawala wa miaka sita wa rais Nicolas Maduro. Rais Trump wa Marekani amesema serikali yake pia inamtambua mjumbe wa kidiplomasia kutoka upande wa upinzani wa Guaido katika ubalozi wa Venezuela nchini Marekani, Carlos Alfredo Vecchio.Mjumbe huyo baada ya kukutana na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence jumanne aliutolea mwito ulimwengu kusaidia kuikomboa Venezuela.
''Tuliweka wazi kwamba hivi vita sio kuhusu itikadi. Hivi ni vita kati ya demokrasia na udikteta. Hivi ni vita kati ya udikteta ambao kwa hali zote unaendeshwa na utawala wa Cuba dhidi ya ulimwengu ulio huru. Hatuwezi kushinda vita hivi peke yetu.Tuna majukumu makubwa kama wavenezuela lakini tunawaomba nyinyi ulimwengu ulio huru kutukomboa kwa namna fulani, Venezuela ambayo iko kwenye ukoloni wa utawala wa Cuba. Kwa hivyo tutaendelea kupambana mpaka tutakapoipata tena demokrasia yetu na ndio sababu tutaendelea kuomba msaada wa Kimataifa''