Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:20 pm

NEWS: RAIA WA RWANDA KUBURUZWA MAHAKAMANI KWA KUJIPATIA MKOPO WA CHUO TANZANIA

IDARA ya Uhamiaji mkoani Kagera inakusudia kuwafikisha mahakamani watu watano akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwagati katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Joseph Kinyonyi, akituhumiwa kushirikiana na wahamiaji haramu hao kuwawezesha wanafunzi wawili wa vyuo vikuu kupata vyeti vya kuzaliwa na kutumia fedha ambazo ni haki ya Watanzania kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Pendo Buteng'e, alisema watakaofikishwa mahakamani mbali na mwenyekiti wa kijiji ni Beatrice Rweyemamu na Frida Kagemlo, ambao walijaza vyeti vya kuzaliwa vya wahamiaji hao kama mama mzazi, pamoja na wanafunzi hao Tumaini Francis anayesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Peace Francis anayesoma Chuo Kikuu cha Mwenge, Moshi.

Buteng'e alisema baada ya uchunguzi walibaini kuwa wanafunzi hao wawili wote ni raia wa Rwanda na kuwa Bukoba kuna mama yao anayeitwa Marie Msabima, anayeishi kwa kibali na anafanya kazi katika Taasisi ya Bethania Christian Aid Foundation iliyoko Kemondo Bukoba Vijijini.

"Tulipochunguza tulibaini wanachuo wote wawili ni ndugu na sio raia wa Tanzania ni raia wa Rwanda, lakini walizaliwa Tanzania na wazazi ambao ni wa Rwanda, wamesoma kuanzia elimu ya msingi, sekondari na sasa vyuo vikuu hapa nchini, walipata vyeti vya kuzaliwa kwa kutoa taarifa za udanganyifu," alisema na kuongeza:

"Katika cheti cha kuzaliwa cha Tumaini majina ya mama yake yanasomeka Beatrice Rweyemamu na Peace majina ya mama yake yanasomeka Frida Kagemlo, na baada ya kupata vyeti vya kuzaliwa walivitumia kuomba mkopo wa elimu ya juu na kupewa wakati hiyo ni haki ya Watanzania," alisema.
Alisema kuwa taarifa za maombi ya mkopo zilithibitishwa na mwenyekiti huyo wa kijiji wakati akijua kuwa taarifa zilizotolewa na wahusika ni za uongo.
Butenge alisema wanakamilisha taratibu ili waweze kuwafikisha mahakamani watu hao watano.


Akijibu tuhuma hizo Mwenyekiti wa Kijiji Kinyonyi, alisema kuwa wakati akiwasainia fomu hakufahamu kama sio raia kwa kuwa aliwaona katika kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Bethania na kudhani wamelelewa hapo kama wanavyolelewa watoto wengine yatima na wa mitaani.