Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 6:10 am

NEWS: POLISI WADHIBITISHA KUMSHIKILIA WAKILI ALBERT MSANDO

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limedhibitisha kumshikilia Wakili na Mfanyabiashara nchini Tanzania Albert Msando kwa tuhuma za kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Serikali kuhusu Ugonjwa wa Corona.

Wakili Albert Msando ashikiliwa na polisi Arusha | Muhabarishaji

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Koka Moita amesema Upelelezi ukikamilika Mtuhumiwa atapelekwa Mahakamani.

Msando alitoa kauli hiyo Jana Aprili 29, 2020 akiwataka waandishi wa habari kote nchini wajitokeze hadharani na kutoa taarifa juu ya ugonjwa wa Corona, huku akitanabaisha kwamba Arusha hali ni mbaya juu ya maambukizi ya virusi hivyo.

Aidha katika hatua nyingine Diwani wa Machame Magharibi kupitia Chama cha Mapinduzi Martin Munisi, amemkosoa Wakili Albert Msando kufuatia kauli yake ya kuwataka waandishi wa habari watoke na kutoa taarifa za Corona na kwamba Arusha hali ni mbaya ili hali hata yeye hakuwa amezingatia tahadhari yoyote.

Diwani Munisi ameyabainisha hayo, alipofanya mazungumzo maalum na kituo cha EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa kauli alizozitoa Msando za kuwa Arusha hali ni mbaya zinaleta hofu kwa wananchi na kwamba kitendo cha kuwataka waandishi wawe mstari wa mbele kutoa taarifa za Corona ni makosa kwa sababu Serikali pekee ndiyo inatoa taarifa za mwenendo wa ugonjwa huo nchini.

"Wakili Msando alikuwa anazungumzia suala la Corona na kugawa vifaa ili hali hata yeye hakuwa amevaa Barakoa, na kile chumba kilikuwa ni kidogo na hakukuwa na tahadhari yoyote, na aliwataka waandishi kukusanya taarifa za Corona na ni wazi kabisa watu wanakufa kwa magonjwa mengine pia" amesema Diwani Munisi.

Aidha Diwani aliendelea kusema "Sasa unapowaambia waandishi waende mtaani ina maana wakikuta mtu anazikwa waandike kafa kwa Corona na alisema hali ni mbaya ili hali na yeye anamiliki Baa ambayo inakusanya watu, ni vizuri tunapozungumzia masuala haya tuwe serious, inabidi tuzungumze mambo tunayoyaishi na uhalisia na kutoleta hofu na vitisho katika jamii".

Novemba 27, mwaka 2017 Msando alijiunga na chama Tawala cha CCM akitokea chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kinachoongozwa na mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akihudumu nafasi ya mshauri wa Chama na Mwanasheria wa chama hicho.

“Nimeona harakati nyingi za serikali na Chama cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo nimekaa nakajitathimini nimeamua kujiunga na CCM ili nisaidie kusukuma gururudumu la maendeleo" alisema Msando baada ya kujiunga na CCM.

Desemba 21, 2017 Rais Magufuli alimteua Wakili huyo kuwa miongoni mwa wajumbe waliokuwa wanaunda tume ya chama cha mapinduzi iliyofatilia na kuhakiki mali za chama hicho.