Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:42 am

NEWS: POLISI KULA SAHANI MOJA NA MADEREVA WA MAGAZETI.

KILIMANJARO: Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amelitaka Jeshi la Polisi kuwa makini na madereva wa magari yanayosafirisha magazeti akisema mara nyingi wamekuwa wakiendesha kwa mwendo kasi.

Mghwira amesema hayo baada ya kuwatembelea kuwajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea wilayani Mwanga ikihusisha gari lililokuwa likisafirisha magazeti.

Katika ajali hiyo, ambayo magari mawili yaligongana uso kwa uso watu wanne walijeruhiwa na wawili wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi wa dereva wa Toyota Hiace ambalo lilikuwa likisafirisha magazeti.

Amesema Hiace lililokuwa likiendeshwa na Godfrey Malisa (37) lilihama njia na kugongana uso kwa uso na Toyota Passo iliyokuwa ikiendeshwa na Ibrahim Mangi (38).

Kamanda Issah amesema katika ajali hiyo iliyotokea jana Ijumaa saa 12:00 asubuhi, majeruhi mmoja mwanamke amevunjika mguu wa kulia na dereva wa Hiace amevunjika mguu na ana maumivu ya kiuno.

Majeruhi Jane Kanyika (31) anayeendelea na matibabu KCMC amesema baada ya gari lao kugongwa lilisukumwa umbali wa mita 100 kutoka barabarani.

Amesema alishtuka baada ya kusikia kilio cha mtoto wake na kwamba wananchi walipofika eneo la tukio kuwasaidia alibaini wanawe wawili walikuwa wamepoteza fahamu.

Kanyika amesema baada ya hapo askari wa usalama barabarani walifika ndipo walipopelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na baadaye kuhamishiwa KCMC.

Dereva Mangi aliyepata maumivu kifuani amesema alishangaa kuona Hiace ikimfuata upande wake na alipojaribu kuikwepa aligongwa na kusukumwa hadi nje ya barabara.