- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: PAPA AINDESHA IBADA YA PASAKA KWA NJIA YA MTANDAO
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francies amelazimika kuvunja utaratibu wa Jumapili ya Pasaka ya miaka yote baada ya kuiendesha misa hiyo kwa njia ya mtandao badala ya kukaa na waumini kutokana na khofu ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Akiendesha ibada hiyo siku ya Jumapili (Aprili 12), ambayo mtu pekee aliyekuwa mbele yake alikuwa mpigapicha wake, Papa Francis alitoa wito kwa walimwengu kutokukubali kutawaliwa na khofu katika wakati huu dunia inapopambana na ugonjwa wa COVID-19, na badala yake watambuwe kuwa "giza na mauti sivyo vyenye kauli ya mwisho."
"Huu sio wakati wa kutofautiana. Kwasababu dunia nzima inataabika na inachohitaji ni kuungana," Papa amesema hivyo katika ujumbe uliopeperushwa moja kwa moja mtandaoni, kutoka katika kanisa la mtakatifu Petro.
Alionya kwamba kuna hatari ya Muungano wa Ulaya kuvunjika na kutoa wito wa kusamehewa kwa madeni kwa nchi masikini.
Ibada za ya Pasaka zimefanyika bila kuhudhuriwa na watu makanisani sehemu mbalimbali duniani wakati ambapo mamilioni ya watu wametakiwa kusalia majumbani.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alitoa baraka zake kwa mji wa Roma na dunia nzima huku amri ya kusalia ndani ikiendelea kudumishwa nchini Italia, moja ya nchi iliyoathirika vibaya na janga la Corona.
Alisema kwamba ujumbe wa pasaka wa mwaka huu ambao umekuwa wa upweke, unatakiwa kuwa wa matumaini, na kusihi viongozi wa kisiasa kushirikiana kwa manufaa ya wote, kusaidia watu katika kipindi hiki kigumu na hatimaye kurejea katika maisha ya kawaida.
"Huu sio wakati wa kuwa wabinafsi kwasababu changamoto iliyopo inakabili kila mmoja," Papa amesema katika ujumbe wake uliojikita zaidi katika athari za mlipuko wa ugonjwa wa corona ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 109,000 kote duniani.
"Kutojali, ubinafsi, migawanyiko na usahaulifu ni maneno ambayo hatutaki kuyasikia kipindi hiki. Maneno haya tunataka kuyakomesha milele," aliongeza.
Bila ya kutaja nchi yoyote, Papa pia alitoa wito wa kulegezwa kwa vikwazo vya kimataifa na kusifu madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine ambao wanaendeleza huduma za msingi.
Kauli ya Papa Francis ilipongezwa na Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, kwa kile alichosema ni ishara yake ya uwajibikaji kwa kuadhimisha Pasaka akiwa faragha.
"Licha ya kuwa maneno yake yametamkwa mbali kutoka Uwanja wa Mtakatifu Petro, ambao kwa sasa umefunikwa na kimya cha kutisha, yamemfikia kila mtu," alisema waziri mkuu huyo wa taifa ambalo lenyewe limeshuhudia vifo vya makumi kwa maelfu ya watu.
Ibada hiyo inayowajumuisha pamoja waumini bilioni 1.3 wa Kanisa hilo ulimwenguni inawakilisha kufufuka kwa Yesu Kristo, ambapo waumini mjini Rome walijaza keki mashuhuri za Pasaka siku kadhaa kabla, kuadhimisha sikukuu yao muhimu.