Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:20 pm

NEWS: OFISI ZA MAWAKILI WA YUSUPH MANJI ZAVAMIWA

Dar es Salaam. Watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo wamevamia na kufanya uharibifu katika Ofisi za Wanasheria wa Prime Attorneys katika jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza Jiji Dar es salaam. Jengo la Prime House lina ghorofa tano lipo jirani na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala. Taarifa zinasema kuwa watu hao wametoweka na kabati la kutunzia nyaraka na fedha za mawakili wa Prime Attorneys.

Mawakili wa (Prime Attorneys) ndio kwasasa wanafanya kazi ya utetezi katika kesi za Mfanyabiashara Yusuph Manji.Mmoja wa mawakili ambao wana ofisi katika jengo hilo, ambaye hakutaka kutaja jina lake aliliambia muakilishi.com leo kuwa watu hao walipofika walimfunga mlinzi kwa kamba na kisha kuingia ndani kwa nguvu.

"Mlinzi ameniambia baada ya kuingia walipokuwa wakifanya upekuzi walikuwa wakisikika wakisema si huku tutazame ghorofa linalofuata si hili,” wakili huyo amemkariri mlinzi.

Wakili huyo amesema, "Sasa nipo njia panda sijui walikuwa wanalenga ofisi gani, kwa vyovyote hawawezi kwenda gym kuchukua vifaa kwa sababu ni vizito nadhani kuna ofisi waliilenga hadi sasa sijajua kwa sababu sijaingia ndani tumekatazwa kuingia.

kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kwenye majira ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo.

"Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa," amesema Kamanda Hamduni.