Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:35 pm

News: "Nilitoa maelekezo kwa Mkandarasi amalize kazi kwa wakati",Waziri Dkt. Kalemani.

DODOMA: Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amefanya ziara ya kukagua miradi ya upanuzi kituo cha kupoza umeme wa kV 220 na mradi wa kituo cha kupoza umeme wa kV 400 eneo la Zuzu.


Lengo la ziara hiyo ni kukagua maelekezo ambayo yalitolewa na Wizara iwapo yametekelezwa.

Dkt. Kalemani amesema hii ni ziara yake ya tatu kwenye mradi huu tangu kuanza kutekelezwa mwezi Machi 2018.


Amesema, katika ziara ya mwezi Novemba mwaka jana alitoa maelekezo kwa Mkandarasi pamoja na wasimamizi wa mradi.

"Mkandarasi alitakiwa kukamilisha Januari 31, mwaka huu, nilitoa maelekezo amalize kazi hizo ndani ya muda na asicheleweshe mradi, baada ya kuona muda umeisha nikaona nije kukagua kama kazi imekamilika, ndio maana nimekuja hapa kufuatilia maelekezo ambayo niliyatoa", amesema Dkt. Kalemani.

Ameongeza, Mkandarasi aliomba nyongeza ya mwezi mmoja kutokana na vifaa kuchelewa Bandarini na aliongezewa muda hadi mwezi Februari mwaka huu.


Aidha, ametoa kwa Mkandarasi Mkandarasi maelekezo mawili la kwanza likiwa ni kuongeza idadi ya wafanyakazi na la pili wafanye kazi usiku na mchana ili waweze kumaliza kazi ndani ya muda waliopewa.

Kukamilika kwa vituo hivyo kutalifanya Jiji la Dodoma kuwa na umeme mwingi zaidi kati ya majiji yaliyopo Tanzania ambapo uwezo wa transfoma utafikia jumla ya megawati 648, huku Jiji la Dar es Salaam likiwa na megawati 587.


Kwa kipindi cha miaka miwili mahitaji ya umeme kwa Jiji la Dodoma yamekuwa yakiongezeka ambapo kwa hivi sasa yamefikia megawati 40.

"Spidi ya kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kwa Dodoma ni kubwa tulikuwa tunabakiwa na megawati takribani 33 lakini hii leo tunabakiwa na megawati 8, hivyo mradi huu unahitajika ukamilike kwa wakati bila kuchelewa", Amesisitiza Dkt. Kalemani.

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa pesa kiasi cha dola za kimarekani milioni 52 kuitekeleza miradi hiyo.