Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 6:01 pm

NEWS: NEC YATOA RATIBA YA UWANDIKISHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA DAR NA PWANI

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imetangaza tarehe ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki ya biometriki (BVR) katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuwa itaanza Ijumaa Februari 14 hadi 20, 2020.

Image result for Jaji Semistocles Kaijage

NEC imesema vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi na kufungwa saa 12 jioni huku ikiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwa na haki ya kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka 2020 ukihusisha madiwani, wabunge na Rais.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage siku za hivi karibuni akizungumza na wadau wa siasa jijini Dar es Salaam alisema uboreshaji wa daftari hilo umefanyika katika mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Dar es Salaam na Pwani.

Jaji Kaijage alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na uchaguzi mkuu mwingine unaofuatia.

Alisema ni matarajio yao baada ya kukamilisha uboreshaji huu wa awamu ya kwanza watakutana tena na wadau kuwafahamisha kuhusu uboreshaji wa awamu ya pili ambao kwa sasa maandalizi yake yanaendelea.

Jaji Kaijage alisema kabla ya kuanza uandikishaji, uhakiki wa vituo vya kuandikisha Wapiga Kura nchi nzima ulifanyika mwaka 2018.

Lengo lake lilikuwa ni kuona kama vituo hivyo bado vipo na kama bado vina sifa na hadhi ya kuwa vituo vya kuandikisha wapiga kura, kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi. Alisema uhakiki huo ulilenga kuangalia iwapo kuna maeneo yanayohitaji kuongeza Vituo.

Kutokana na uhakiki huo, vituo vya kuandikisha wapiga kura kwa nchi nzima viliongezeka kutoka vituo 36,549 hadi 37,407.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam Vituo hivyo viliongezeka kutoka 1,614 vya kuandikishia wapiga kura vilivyokuwapo mwaka 2015, hadi kufika vituo 1,661 mwaka 2020. “Ni vituo 47 tu vya uandikishaji wapiga kura vilivyoongezeka katika Mkoa huu wa Dar es Salaam,” alisema Jaji Kaijage