Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:48 am

NEWS: NEC YATENGA SIKU 3 KUHAKIKI KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

Dar es Salaam. Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imesema uboreshaji wa daftari la wapiga kura awamu ya pili wanapanga kuanza mwezi Aprili 17 hadi Mei 4, mwaka huu ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu ujao hapa nchini.

Ratiba hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 8, 2020 na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage katika ufunguzi wa kikao cha tume hiyo na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa.

Jaji Kaijage amewataka wananchi Wote waliojiandikisha mwaka 2015 na awamu ya kwanza mwaka 2020 kujitokea katika kipindi hicho kilichotolewa cha siku tatu kila eneo kuhakiki taarifa zao au kuwawekea pingamizi wapiga kura wasiokuwa na sifa.

Lengo la mkutano huo ni kutoa maelezo ya kikao kama hicho kilichofanyika Machi 23, 2020 kujadili uboreshaji wa daftari hilo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2020.

Jaji Kaijage amesema awali uboreshaji ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu lakini kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishw ana virusi vya corona, wamepunguza na utafanyika katika awamu mbili.

Amesema tume imenunua vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya corona ikiwamo barakoa, vitakasa mikono, ndoo za maji ya kunawa na maofisa wao watakuwa kila eneo la uandikishaji kuwapanga watu ili kuepuka msongamano.

"Vituo vitakuwa kila kata na uboreshaji utakuwa siku tatu na awamu ya kwanza itahusu mikoa 12 ya Tanzania bara kuanzia Aprili 17 hadi 19,2020," amesema Jaji Kaijage

Ametaja mikoa ni; Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.

Mwenyekiti huyo amesema awamu ya pili itaanza Mei 2 hadi Mei 4,2020 katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ni Katavi, Singida, Mbeya, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Rukwa.

Jaji Kaijage amesema katika kipindi hicho wananchi waliokwisha kujiandikisha wanapaswa kuhakiki taarifa zao kwa kufika vituoni.

Amesema mwananchi anaweza kuhakiki kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa kubonyesha *152*00# na kufuata maelekezo au kutembelea tovuti ya tume au kupiga simu kituo cha wapiga kura kwa namba 0800782100 bure.

Jaji Kaijage amesema hata idadi ya vituo vya kuandikishia vimepungua kutoka 8031 hadi 4006.