Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:24 am

NEWS: NCHI YA HISPANIA MBIONI KUGAWANYIKA BAADA YA KURA YA MAONI

Barcelona: Leo Wacatalonia wamepanga foleni tayari kupiga kura ya maoni ya kutaka kujitenga kwa jimbo hilo lililopo nchini hispania, kura hiyo ambayo iliyopigwa marufuku na serikali kuu ya Uhispania. Shirika la habari la Reuters limeripoti mamia wamejitokeza katika vituo kadhaa vya kupiga kura Barcelona.

Msafara wa malori karibu 100 ya polisi, yameondoka kutoka bandari ya Barcelona leo asubuhi. Maelfu ya polisi wametumwa mjini humo kutoka kila pembe ya Uhispania kuzuia kura hiyo ya maoni kutofanyika.

Mahakama za Uhispania ziliamua kuwa kura hiyo ya kujitenga kwa jimbo la Catalonia inakiuka katiba na serikali kuu imejaribu kutumia kila mbinu za kisheria kuzuia isifanyike. Kufuatia maagizo ya majaji na waendesha mashitaka, polisi imechukua karatasi za kupigia kura, kuwakamata waandaaji wakuu wa kura hiyo na kuifunga mitandao ambayo inatetea kura hiyo yenye utata.

Jimbo hilo la Catalonia lililo kaskazini mashariki mwa Uhispania lenye utajiri mkubwa na lina idadi ya watu milioni 7.5. Utajiri wa jimbo hilo ni mkubwa kuliko wa nchini ya Ureno.

Wizara ya mambo ya ndani imesema siku ya Jumamosi, polisi ilifunga takriban vituo 2,315 vya kupigia kura katika jimbo hilo. Hata hivyo vituo 160 vilikaliwa na watu wakiwemo, walimu, wazazi, wanafunzi na wanaharakati ambao wamepania kuhakikisha vinasalia wazi ili watu waweze kupiga kura.