Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 10:21 am

NEWS: NCHI INATAHARUKI BAADA YA CHADEMA NA ACT KUSUSIA UCHAGUZI

Chama kingine cha upinzani chenye ushawishi nchini Tanzania cha ACT Wazalendo chenye udhibiti mkubwa Tanzania visiwani kimejitoa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa wa nchi hiyo kikiunga maamuzi yaliyofanywa na chama kikuu cha Upinzani Chadema.

Vyama hivyo vimejitoa katika Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanywa 24 Novemba 2019.

''Takribani, wananchi 173,593. Hata hivyo, kati ya wagombea wetu hao 173,593 waliochukua na kurejesha fomu za uteuzi, 166,649 walienguliwa katika mchakato wa Uchaguzi nchi nzima kwa sababu mbalimbali za kipuuzi na zisizo na mashiko kabisa kama ilivyoelezwa na Viongozi wetu katika nyakati mbalimbali za mchakato huu. Wanachama wa ACT waliobakizwa kwenye Uchaguzi mpaka saa Sita kamili mchana leo ni 6,944 tu sawa na 4% ya wagombea wote tulioweka.'' Anasema Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT wazalendo katika mkutano na waandishi wa habari.

Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Taifa kilikutana Jana kujadili hali na mwenendo wa uchaguzi huo nchini Tanzania.

Lakini pia chama hiko kimedai kutumika vibaya kwa jeshi la polisi la nchini Tanzania kuingia mchakato wa uchaguzi huo.

Sasa uchaguzi umekosa ushawishi kwakuwa vyama shindani nchini humo vimejitoa katika Uchaguzi huo.

Huenda taifa hilo likashuhudia idadi ndogo sana ya watu watakaojitokeza kupiga kura hapo novemba 24 mwaka huu.

Zitto Kabwe alitoa uwamuzi huo jana mara baada ya chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema kutangaza kuwa kimejitoa katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Aidha serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi imesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika kama ulivyopangwa tarehe 24 mwezi Novemba mwaka huu.

Ufafanuzi huo umetolewa mapema hii leo katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni, Dodoma ambapo Mbunge wa Singida Kaskazini Justice Monko alitaka ufafanuzi wa serikali hasa baada ya Chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania Chadema kutangaza kujitoa rasmi katika mchakato wa Uchaguzi huo.