Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 11:52 am

NEWS: NAPE AWACHONGEA WAKANDARASI KUTOKAA SEHEMU ZAO ZA KAZI

Dodoma: MBUNGE wa Mtama,Nape Nnauye (CCM) amewachongea wakandarasi ambao hawakai sehemu zao za kazi na badala yake wamekuwa wakifika katika maeneo ya kazi pale tu wanapokuja wageni wa kiserikali.

Nape alitaka kujua ni hatua gazi ambazo serikali itawachulia wakandarasi hao kutokana na vitendo vya kutokaa katika maeneo ya kazi jambo ambalo alieleza kuwa linachelewesha miradi mingi ya maendeleo.

Akiuliza swali la nyongeza Bungeni Nape aliihoji serikali ni hatua zipi ambazo serikali itawachulilia wakandarasi hao ambao wamekuwa wakichelewesha miradi mingi ya maendeleo kutokana na kutokaa katika maeneo yao ya kazi tofauti na mikataba yao inavyoelekeza.

Awali katika swali la msingi la mbunge wa Lindi Mjini,Hassani Kaunje, (CCM)alitaka kujua ni lini serikali itatimiza ahadi ya rais wa awamu ya tano ili kuondoa adha ya tatizo la maji kwa wananchi wa jimbo hilo.

“Mradi wa Ng’apa ukikamilika utawahudumia wakazi wa Lindi mjini, mradi huo ulipaswa ukamilike tangu mwezi Mei 2015 lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika.

“Je ni lini serikali itatimiza ahadi ya Mhe, Rais ya kuondoa adha ya tatizo la maji kwa wananchi wa Lindi mjini” alihoji Kaunje.

Akinibu maswali hayo Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Isack Kamwelwe,alisema kuhusu swali la Nyongeza la Nape,alilieleza bunge kuwa wakandarasi ambao wanaondoka katika maeneo yao ya kazi wanakiuka mikataba yao jinsi inavyowaelekeza.

Aidha alisema ni wajibu wa wale ambao wanasimamia mikataba kusimamia mikataba hiyo ili kuhakikisha miradi mingi inayofanyika inatekelezwa kwa kiwango na kwa muda unaokubalika kadri ya mkataba unavyoelekeza.

Akijibu swali la msingi la mbunge wa Lindi mjini, Kamwelwe alisema kuwa mradi wa Ng’apa unagharamiwa na serikali kwa kushirikiana na umoja wa Ulaya (EU) kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW kwa gharama ya EURO milioni 11.56.

Aidha alisema kuwa kuchelewa kumaliza kwa mradi huo ni kutokana na kutolipwa kwa wakati fidia na kasi ndogo ya mkandarasi katika ujenzi wa mradi huo.