Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:47 pm

NEWS: MWANDISHI KABENDERA AMEPOOZA MGUU NA ANASHINDWA KUPUMUA VIZURI

Upande wa utetezi Ukiwakilishwa na Wakili Jebra Kambole katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kulielekeza Jeshi la Magereza kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili mtuhumiwa ili aweze kupatiwa vipimo.

Wakili Kambole pia amesema kuwa afya ya Kabendera ianendelea kuzorota baada ya kupata tatizo la upumuaji inapofika usiku tangu Agosti 21 hali iliyomfanya kushindwa kutembea kwa siku mbili.

Wakili Kambole amedai usiku wa kuamkia Agosti 2, 2019 mteja wake akiwa gerezani alianza kuumwa na hadi leo ana shida ya kupumua

''Kwa kuwa mteja wetu hajapata huduma ya matibabu tunaomba Mahakama ielekeze maafisa wa magereza kumpeleka katika hospitali yoyote ya serikali akapimwe '' alisema wakili huyo.

"Kwa kuwa mteja wetu hajapata vipimo ambavyo vinastahili tunaomba Mahakama ielekeze Jeshi la Magereza mteja wetu akapimwe katika hospitali yoyote ya serikali ikiwemo Muhimbili penye vipimo vya uhakika," amedai Wakili Kambole

Hata hivyo Wakili wa Serikali, Simon Wankyo ameipinga hoja hiyo kwa kudai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina Mamlaka ya kutoa amri yoyote ile isipokuwa Mahakama kuu.

"Mahakama yako haiwezi kuamuru kupelekwa hospitali fulani kwa kuwa hajawahi kuwasilisha maombi akakataliwa lakini sheria inasema makosa ya uhujumu uchumi yanasikilizwa na Mahakama Kuu hivyo Mahakama hii haina uwezo wa kutoa uamuzi wowote" ameeleza Wakili Wankyo

Aidha Hakimu Rwizile ambaye anasikiliza Kesi hiyo amepata udhuru na kushindwa kufika mahakamani hapo.Kabendera ambaye ni Mwandishi wa kujitegemea aliyekuwa akichapisha habari zake katika vyombo mbalimbali nchini na ulimwenguni alikamatwa nyumbani kwake Mbweni, viungani mwa jiji la Dar es Salaam na watu wanaodhaniwa kuwa ni maafisa wa polisi mnamo Julai 29, 2019.

Kabendera alipandishwa kizimbani Agosti 5 na kusomewa mashtaka matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi .

Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar Es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.